Monday, December 31, 2012

MHESHIMIWA MNYIKA


Wakazi wa Kata ya GOBA: Tume ya Haki za Binadamu imetangaza/imenukuliwa kwenye vyombo vya habari leo kuwa imeanza kuchunguza na kuchukua hatua juu ya mashtaka niliyowasilisha kuhusu mgogoro wa toka mwaka 2007 unaokwamisha huduma ya MAJI katika mtaa wa Goba. Kwa upande wa Mtaa wa Kulangwa-Kata ya Goba tenki limeshajengwa, ujenzi wa miundombinu mingine unakaribia kuanza ili wananchi wapate maji kupi...tia mradi wa Madale Kisauke. Ili kuwa na usimamizi bora kuanzia hatua za awali fikeni leo (Desemba 30, 2012) kuanzia saa nane mchana , Mahali: Shule ya Kulangwa kutoa maoni kuhusu Katiba ya Jumuiya ya watumiaji Maji. Tume ya Haki za Binadamu a Utawala Bora ayo ikifika muipe ushirikiano tupate ufumbuzi wa kudumu. Pamoja na jumuiya za watumiaji wa maji na kamati za maji kama ufumbuzi wa mpito, suluhisho la kudumu ni Kata nzima ya GOBA kuhudumiwa moja kwa moja na DAWASA na DAWASCO kupata miundombinu inayoendana mijini kwa kuwa Goba si kijijini tena.
Hakika Tutafika!

HILARY CLINTON ALAZWA HOSPITALINI

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton amelazwa hospitali kutokana na kuganda kwa damu baada ya kuumia kichwani hivi karibuni.

Wizara ya mambo ya nje inasema madaktari wa Clinton waligundua hali hiyo jana jumapili  alipokwenda kwenye uchunguzi wa kawaida. Wamesema ilikuwa inahusiana na kujigonga kichwani baada ya kuanguka wiki kadhaa zilizopita.

Clinton anatibiwa na dawa za kusaidia damu kutokuganda katika hospitali ya Presbyterian huko New York. Anategemewa kubaki hospitali kwa uangalizi zaidi kwa siku mbili zijazo.

Taarifa imesema madaktari wa Clinton wataendelea kumwangalia na kuangalia kama kuna haja ya kuchukua hatua zaidi
                                                                                                                                                      

Saturday, December 29, 2012

WAIMBAJI WA GOSPEL NCHINI WAPATA AJALI MBAYA MLIMA KITONGA

Waimbaji wa muziki wa injili nchini Pascal Cassian (mshindi wa Bongo star search)pamoja na Lembo junior ambaye ametamba na wimbo Tutembelee juzi walipata ajali mbaya ya gari katika mlima Kitonga mkoani Iringa kwa gari ndogo waliyokuwa wakisafiria kutoka jijini Mbeya kwenda Dar es salaam kupinduka mara tatu baada ya breki kushindwa kufanya kazi lakini Mungu akawaepushia kifo.

Katika ujumbe aliomtumia mtangazaji wa Wapo Radio Fm 98.1, Silas Mbise, Lembo amesema kwa jinsi ajali hiyo ilivyotokea ilikuwa wote wafariki duniani lakini Jehovah amewatetea na kutoka salama ingawa mmoja kati ya watu 6 waliokuwemo katika gari hiyo Gastor Sapula damu zilikuwa zikimtoka mdomoni huku Lembo akisikia maumivu katika bega lake.

 Ukiacha Lembo na Pascal watu wengine waliokuwemo kwenye gari hiyo ni pamoja na mwinjilisti Jailos Maloda, Gastor Sapula pamoja na vijana wengine wawili waliokuwa sambamba na Pascal kwa uimbaji katika huduma waliyoifanya jijini Mbeya.




 
Source:gospelkitaa.blogspot.com

KAA TAYARI NA UJIO MPYA WA ROMA

Huu ndio Ujio Mpya wa Msanii Roma kaa Tayari Kuupokea msikilize

UFARANSA YAKATAA OMBI



Ufaransa imekataa ombi la rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize kusaidia kuwarudisha nyuma waasi wanaotishia kuiangusha serikali yake, huku Marekani ikiamua kufunga ubalozi wake nchini humo.
Wasiwasi umezidi kutanda nchini humo wakati muungano wa waasi hao unaojulikana kama Seleka ukizidi kusonga mbele kuelekea mji mkuu Bangui, kwa madai kuwa serikali imekiuka makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka 2007. Lakini rais Francois Hollande wa Ufaransa amekataa ombi la rais Francois Bozize akisema kuwa muda wa kufanya hivyo ulikwisha.
Wakati huohuo,Marekani kwa upande wake imetangaza jana Alhamisi kuwa inasitisha shughuli zote katika ubalozi wake mjini Bangui, na kwamba balozi wake na wafanyakazi wengine wa ubalozi huo walikuwa wameondoka nchini humo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Patrick Ventrell, alisema uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi hao, na kwamba hatua hiyo haihusiani kwa namna yoyote ile na uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili. Marekani pia iliwatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Hayo yanajiri wakati viongozi wa kanda hiyo wakijaribu kuratibu makubaliano ya kusitisha mapigano na waasi walikuwa wamesema wamesimamisha kwa muda, operesheni kuelekea mji mkuu, ili kuruhusu mazungumzo kufanyika. Waasi hao wanataka serikali itekeleze makubaliano ya kuwatawanya na kuwaingiza katika maisha ya kiraia.
"Wapiganaji wanataka pesa walizoahidiwa ili kuweza kujiunga na jamii ya kiraia, programu ya kuwatawanya ilihusu kuwanyang'anya silaha wapiganaji lakini yote hayo hayakutekelezwa na ndiyo matatizo makubwa. Lingine ni kuundwa kwa ajira kwa waasi kwa lengo la kuwaingiza katika maisha ya kiraia," alisema Thierry Vircoulon kutoka shirika la kutatua migogoro la International Crisis Group, anafafanua madai ya waasi hao.

MWILI WA MWANAMKE ALIYEBAKWA WARUDISHWA INDIA

Mwili wa mwanamke wa India ambaye amefariki hospitalini nchini Singapore baada ya kubakwa kinyama mjini New Delhi utarejeshwa kwa ndege maalum ya kukodi baadaye leo Jumamosi(29.12.2012).
Balozi  wa  India  nchini  Singapore T.C.A Raghavan  amewaambia waandishi  habari, saa  kadha  baada  ya  mwanamke  huko  kufariki kutokana  na  viungo  vyake  kushindwa  kufanya  kazi  katika hospitali  nchini  Singapore  ambako  alikuwa  akipatiwa  matibabu.
Mwanamke  huyo  na  ndugu  wa  marehemu  watasafirishwa kwenda  India   katika  ndege  maalum  ya  kukodi  baadaye  mchana wa  leo  Jumamosi, (29.12.2012) , amesema  Raghavan.

Friday, December 28, 2012

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA TFF


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 28, 2012
Klabu 14 ambazo timu zao zinashiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesema hazitacheza hatua ya pili ya Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh. 157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za Taifa.
Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya makocha hao moja kwa moja kwenye akaunti zao, lakini ilikuwa haikati PAYE kutoka kwenye mishahara hiyo, hivyo malimbikizo kufikia sh. 157,407,968.
TFF bado inaendelea na mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.
OFISA WA CAF KUTUA MWAKANI KUKAGUA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo.
Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.
Utekelezaji wa kazi yake nchini utahusisha mwakilishi kutoka TFF, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mameneja wa viwanja husika na Ofisa Usalama wa TFF.
NAZARIUS KILUNGEJA AONDOLEWA UCHAGUZI RUREFA
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa Nazarius Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.
Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa awali.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Goldie Ft. AY - Skibobo [Official Video]

AY - Money [Official Video]

KUTOKA KWA MB.JOHN MNYIKA


Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha Sheria
 ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.
Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.
Pendekezo hilo lingeliwezesha Bunge kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa.

Kutokana na Serikali kutokuzingatia pendekezo hilo na badala yake Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa mradi huo tarehe 8 Novemba 2012 Mkoani Dar es salaam huku usiri ukiendelezwa malalamiko yameanza kujitokeza katika maeneo ya mradi husika hususan katika Mkoa wa Mtwara.

Aidha, Serikali irejee katika mapendekezo niliyotoa bungeni na kutoa maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi huo na miradi mingine inayopaswa kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa maendeleo ya wananchi husika.

Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Serikali inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).

Kwa upande mwingine, utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila kuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na kuisimamia Serikali hivyo ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na barua niliyomwandikia mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa haijajibiwa.

Ikumbukwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine nilipendekeza Spika aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi asili.

Hatua hii ni muhimu kwa sasa kwa kuwa hata baada ya uamuzi wake kuhusu tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati husika, Spika hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa hali ambayo imeacha ombwe la uongozi na usimamizi wa kibunge (Parliamentary Oversight) kwenye sekta hizi nyeti kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

TABLETS KUTOKA AFRIKA


MFANO WA TABLET ZA VIM KUTOKA AFRIKA

Simu aina ya smartphone na kompyuta za tablet zinazosemekana kuwa vifaa vya mawasiliano vya kwanza kutengenezwa na kampuni ya Afrika zimezinduliwa.
Vifaa hivyo, ambavyo vimebuniwa na mjasiriamali wa Congo,vinatengenezwa nchini China.
Kampuni yake ya VMK, vifaa vyake vinaendeshwa kwa teknolojia ya Android ya Googles.
Simu hizo za smartphone zitauzwa kwa bei ya rejareja ya dola $170, sawa na pauni za Uingereza (£105) na kompyuta itauzwa kwa dola $300 sawa na pauni (£185).
"Ni Waafrika wenyewe, ndiyo watakaofahamu mahitaji ya Afrika," amesema Bwana Mankou katika mkutano wa Tech4Africa mjini Johannesburg.
"Apple ni kampuni kubwa Marekani, Samsung ni barani Asia na tunataka VMK kuwa kampuni kubwa barani Afrika."
Blogu ya teknolojia ya Smartplanet imeripoti kuwa kompyuta za VMK zinatoa huduma ya uunganishaji wa wi-fi na uwezo wa gigabytes 4 ambazo zimehifadhiwa ndani yake.
Verone Mankou, ndiye aliyeunda kifaa hiki
Jina lake, Way-C, lina maana ya "mwanga wa nyota" katika lugha ya Kilingala.
Simu hiyo ya smartphone nyuma na mbele ina kamera na skrini ya ukubwa wa inchi 3.5 sawa na sentimita 8.9.
Kuna mipango ya kuuza simu hizi katika nchi kumi za Afrika Magharibi pamoja na Ubelhiji, Ufaransa na India.
Bwana Mankou amesema anatarajia kuzindua uuzaji wa kompyuta za bei nafuu zaidi kwa wanafunzi mwaka ujao.
VMK imesisitiza kuwa wakati bidhaa zake zinatengenezwa China kwa sababu za unafuu wa gharama, ubunifu na uhandisi wa simu hizo ni wa Kiafrika.
Hii ni kutokana na baadhi ya watu au kampuni za biashara kupinga uwezo wa kampuni hiyo katika teknolojia ya simu na kompyuta.
Kampuni ya VMK imesema kinyume na bidhaa nyingine za awali za simu na komputa zilizosemekana kuwa za Afrika, bidhaa za VMK hazifanani na bidhaa zozote za aina hiyo katika nchi nyingine.

Habari kwa Hisani ya BBC-Swahili

MANDELA ARUHUSIWA KUTOKA HOSPITALINI



Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela, ameruhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitali moja mjini Pretoria.
Ikulu ya rais nchini humo imesema rais huyo wa zamani wa Afrika kusini, anaendelea kupata nafuu nyumbani mwake.
Msemaji wa serikali amesema Mandela bado hajapona kabisa na ataendelea kupokea matibabu nyumbani mwake mjini Johannesburg.
Mandela alilazwa hospitaini siku kumi na nane zilizopita kufuatia maambukizi ya mapafu
Mkewe Graca Machel, na rais Jacob Zuma walimtembelea Bwana Mandela siku ya Krismasi na walisema kuwa alikuwa katika hali nzuri.
Baada ya ziara hiyo, rais Zuma alisema kuwa madaktari wamefurahishwa na jinsi Bwana Mandela alivyokuwa akiendelea kupona kwa haraka licha ya umri wake.
Rais Zuma aliwashukuru raia wa nchi hiyo kwa sala zao za heri njema kwa rais huyo wa zamani.
Hata hivyo aliomba raia na waandishi wa habari kuwa na subira na wakati huo huo kuwapa bwana Mandela na familia yake nafasi wanayohitaji.
Hii ni mara ya kwanza tangu mwaka wa 1990 ambapo rais Mandela amelazwa hospitalini kwa muda mrefu zaidi.
Mjuu wa Bwana Mandela, Mandla, amesema, kutokuwepo kwa babu yao wakati wa Krismasi kumewasikitisha sana kwa sababu hawakudhani kuwa angesalia hospitalini kwa muda huo wote.