Wednesday, January 9, 2013

CCM yakanusha tuhuma za Chadema


Nape Mnauye msemaji wa Chama cha Mapinduzi

SIKU moja baada ya Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), kudai CCM inashirikiana na baadhi ya viongozi wake kukisaliti chama hicho, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amekanusha tuhuma hizo.
Nape alisema CCM haihusiki na mgogoro wowote ndani ya chama hicho, hivyo wanapaswa kumtafuta mchawi wao siyo kukilaumu chama chake.
“Mchawi wanaye wenyewe ndani ya chama chao, hatuhusiki na lolote hivyo wanapaswa kujipanga na kuulizana kubaini tatizo linalowasumbua,” alisema.


Aliongeza kuwa CCM haina muda wa kuhujumu chama hicho, ila wana muda wa kutekeleza ilani za chama maeneo mbalimbali nchini.


Nape alisema kutokana na hali hiyo, CCM imejipanga kuhakikisha ahadi zinatekelezwa kwa vitendo, ikiwamo maazimio yaliyotolewa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho.
Baadhi ya viongozi wa Bavicha wanaodaiwa kushirikiana na CCM kudhooficha Chadema na wengine walifukuzwa uanachama.


Miongoni mwa viongozi hao ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Juliana Shonza, Habib Mchange, Mtera Mwampamba, Gwakisa Burton na Joseph Kasambala.


Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment