Monday, January 14, 2013

Mwenyekiti Sau aiangukia Serikali



MWENYEKITI wa Chama cha Sauti ya Umma (Sau), Paul Kyara ameiomba Serikali imsaidie aende kupatiwa matibabu nchini India kutokana na tatizo la kibofu linalomsumbua kwa muda sasa.
Amesema tatizo hilo limesababisha figo kushindwa kufanyakazi vizuri na kumfanya awe na msukumo mkubwa wa damu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kyara alisema kwa kipindi kirefu sasa anasumbuliwa na tatizo hilo na miezi miwili iliyopita alikuwa katika hali ambayo si nzuri.
“Nilikuwa katika hali mbaya sana, lakini namshukuru Mungu kwa sasa na ninaiomba Serikali inisaidie kwenda nje kupata matibabu,’’ alisema.
Alisema kuwa anapata matibabu na kuna baadhi ya vipimo anavisubiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na ile ya Regency, lakini hali haijamruhusu walau kufanya shughuli zake za kila siku ikiwa ni pamoja na zile za chama.
“Ninaendelea vizuri, lakini siyo sana isipokuwa ninasubiri vipimo, ili nisikie madaktari wanasemaje, lakini kimsingi nahitaji matibabu zaidi,” alisema Kyara na kuongeza kuwa ingekuwa vizuri kama Serikali ikawa na utaratibu wa matibabu pia kwa viongozi wa kitaifa wa vyama badala ya kuwa kama ilivyo sasa.
Alisema Serikali inawatazama zaidi wabunge, lakini hata wao ni watumishi wa nchi na hata hao wabunge wanatokea katika vyama ambavyo wao wana viongozi, hivyo litakuwa jambo zuri kwao pia kusaidiwa kwani gharama za matibabu zipo juu na ni wachache ambao wanaweza kumudu.
Mwenyekiti huyo ambaye pia ni kiongozi anayemaliza muda wake katika vyama visivyo na wabunge bungeni katika Kituo cha Demokrasia (TDC), alisema licha ya yeye kuna wenyeviti wengine saba wa vyama tofauti ambao wanasumbuliwa na maradhi mbalimbali na hawana msaada wa maana.
“Siyo mimi tu bali pia kuna wenyeviti wengine saba wa vyama vya upnzani ambao wanaumwa isipokuwa kila mmoja ataizungumzia nafsi yake kwanza ndiyo maana naomba huo msaada,” alisema na kuongeza kuwa utaratibu ukiwapo wa matibabu kwa wenyeviti itakuwa jambo jema.
Mwenyekiti huyo kwa miezi miwili sasa anaugulia nyumbani akisumbuliwa na tatizo hilo la kibofu ambalo sasa limesababisha figo kushindwa kufanya kazi vizuri pia ugonjwa wa shinikizo la damu.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment