Friday, January 18, 2013

Simba mazoezi, kula, kulala Oman


KOCHA wa Simba, Patrick Liewig anasisitiza mambo matatu makubwa kwa wachezaji wake katika kambi ya timu hiyo hapa Oman ambayo ni mazoezi, kula na kulala.
Simba imejichimbia katika Mji wa Muscat eneo la Ghalla kwenye Hoteli ya Al Madinah Holiday yenye gym ya kufanyia mazoezi pamoja na bwawa la kuogelea ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya Ligi Kuu pamoja na michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mfaransa Liewig alisema,”unapofika katika hoteli hii hauwezi kuona mchezaji anang’aa macho nje, ukiona hivyo tu ujue wako safarini kwenda mazoezini au wametoka kwa ajili ya kupata chakula.”
Alisema wachezaji wanatakiwa kusimamia mambo matatu ambayo ni mazoezi, kula na kupumzika vya kutosha ili waweze kucheza soka vizuri.

‘’Nataka wachezaji kufuata maelekezo bila kupindisha kitu ili kufanikisha tulichokikusudia kwa sababu sisi ni timu,’’ alisema Liewig.
Kocha huyo amewawekea ratiba kabisa na maagizo yote juu ya programu ambayo yameandikwa katika ubao ili kila mmoja apate maagizo hayo kwa kusoma.
Mazoezi
Hadi jana ilikuwa ni kipindi cha sita tangu watue hapa, hawajawahi kupumzika na ratiba yao ya mazoezi wanafanya asubuhi na jioni.

Simba hufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Seeb unaomilikiwa na Chama cha Soka cha Oman, umbali wa kilomita 2 kutoka ilipo hoteli wanayokaa Simba.
Mara nyingine hutumia Uwanja wa Fanja ambao uko umbali wa dakika 30 kwa mwendo wa gari.
Katika mazoezi hayo, Mfaransa huyo amekuwa akifanya ufundi wake na kuwasisitizia umakini katika kutoa pasi au kupokea pamoja na ushambuliaji.

Kulingana na idadi ya wachezaji waliopo, wanafanya mazoezi kama wako wengi huku wakitumia uwanja mzima akiwa na lengo la wachezaji kupata stamina.
Liewig alisema hii ndiyo kazi iliyowaleta na lengo ni kutengeneza kikosi bora cha mashindano.

Ratiba ya mechi
Simba inatarajia kuanza ratiba ya mechi kuanzia Januari 16 baada ya wachezaji wote kukamilika.
Wakati huohuo; Wachezaji Ramadhani Singano na Abdalah Seseme wameshatua kambini Oman, huku wale waliokuwa na Taifa Stars wakitegemewa kuwasili wakati wowote mjini Muscat.

Taifa Stars ina wachezaji sita wa Simba ambao ni Juma Kaseja, Amri Kiemba, Shomari Kapombe, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto na Amir Maftah waliokuwa na Stars nchini Ethiopia ambako walikuwa na mechi ya kirafiki juzi Ijumaa na wakafungwa 2-1.
Mwenyeji wa Simba hapa Oman, Talib Hilal aliliambia gazeti hili kuwa, ratiba ya wachezaji hao imebadilika na sasa watawasili hapa wakitokea Dar es Salaam.

‘’Hadi Jumatatu tunatarajia wachezaji wote watakuwa wamekamilika,  wale wachezaji wa Simba ambao wapo katika kikosi cha Stars wataungana na wenzao wakitokea Dar es Salaam na siyo Addis Ababa kama ilivyokuwa awali,’’ alisema Talib.

No comments:

Post a Comment