Thursday, February 28, 2013

Gharama ndogo za simu kuongeza masoko na wateja

MKAZI wa jijini Dar es Salaam, Hija Omar analazimika kutumia wastani wa Sh5,000 kwa siku kwa ajili ya mawasiliano ya simu kutokana na kipato chake. Omar anafanya ya kuuza matairi ya pikipiki ya magurudumu matatu.
 Bila kufanya hivyo anaweza kupoteza wateja wake ambao wanategemea chombo hicho kuwafikisha maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam ambako teksi haziwezi kufika kirahisi.
 Omar ana kazi zaidi ya moja na mitandao mitatu tofauti ya simu za mkononi inayomsaidia kuwasiliana na wateja wake.
 “Ninakwepa gharama za kuwasiliana, wateja wangu ambao wapo mitandao  tofauti , siwezi kutumia laini ya voda au Airtel kuwasiliana na mteja wa Tigo.
 “Hata kama mtu ‘akinibipu’ ni rahisi kumpigia hii ndiyo sababu nalazimika kutumia laini zaidi ya mbili,” anasema dereva huyo wa Bajaj.
 Kadhia ya kuwa na laini zaidi ya moja inayomsibu Hija huenda ikamalizika kesho, baada ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (Tcra) kushusha gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine. Tcra imeshuka gharama za siku kutoka Sh115 mpaka Sh34.92 kwa dakika moja.
 Hii ni habari njema kwa Hija na watumiaji wengine wa simu za mkononi ambao kwa mujibu wa taarifa za Tcra mpaka kufikia Septemba, mwaka jana kulikuwa na watumiaji wanaokadiriwa milioni 23.8 waliosajiliwa sawa na asilimia 93 ya watumiaji wote waliosajiliwa kutoka kampuni saba za simu za mkononi nchini.
Tcra ilifanya mabadiliko hayo baada ya kupitia gharama za mwingilio wa kampuni za simu na kuweka punguzo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tcra, Profesa John Nkoma anasema wameshusha gharama hizo ili watumiaji wa simu wawe huru kupiga simu kwenda mtandao wowote.
 Anasema gharama mpya zitawaondolea Watanzania mzigo wa kubeba laini nyingi za mitandao tofauti.
 Profesa Nkoma anasema uamuzi wa kushusha gharama za mwingiliano wa mawasiliano ya simu za mkononi itakuwa sheria ambayo kampuni zote za simu zitalazimika kuzitekeleza.


Source :Mwananchi

No comments:

Post a Comment