Friday, February 15, 2013

Spika aongezewa ulinzi

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda ameongezewa ulinzi pamoja na kubadilishiwa namba za gari analotumia kutokana na vitisho anavyovipata kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa simu.
Taarifa ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya viongozi wa Chadema kutoa namba za Spika na kuzigawa kwa wafuasi wake waliofika kwenye mkutano uliofanyika kwenye Viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam hivi karibuni ili wamtumie ujumbe mfupi wa simu.

Hivi karibuni gazeti hili liliripoti kuwa Spika Makinda amepokea ujumbe mfupi wa simu zaidi ya 400 na kupigiwa simu zinazofikia 200 za kumkashifu na vitisho.
Taarifa zilizopatikana jana zinaeleza kuwa Spika Makinda amekuwa akitumiwa ujumbe mfupi wa vitisho ambavyo inaonyesha kuwa wananchi wana hasira naye na ndiyo maana ameongezewa ulinzi.

Vyanzo vyetu vya habari vimeeleza kuwa gari la Spika Makinda limebadilishwa namba kwa kuondolewa herufi S ambayo humaanisha Spika na kuwekwa namba nyingine ambazo bado hazijajulikana.

“Watu wanaomtumia ‘meseji’ wana hasira, wanaweza kumdhuru na ndiyo maana ameongezewa ulinzi. Hata magari yake aliyokuwa akitumia yamebadilishwa na kupewa mengine tofauti,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Spika Makinda mwenyewe alipopigiwa simu ili kueleza kuhusu suala hilo la kuongezewa walinzi simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah naye simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.Tangu Chadema wagawe namba hiyo baada ya kumtuhumu Spika pamoja na msaidizi wake, Job Ndugai kuwa amekuwa akipindisha kanuni wakati wa kuliongoza Bunge.

Taarifa zilieleza kuwa wamekuwa wakisumbuliwa na kutumiwa ujumbe za vitisho.Wakati hayo yakitokea, tayari Ofisi ya Bunge imesema itawachukulia hatua kali wale wote waliotumia lugha chafu kwa ujumbe mfupi ama kupiga moja kwa moja kwa Spika na Naibu wake.

Katibu Mkuu wa Bunge, Dk Kashililah juzi alisema kuwa kutoa namba si tatizo, bali kuzitumia namba hizo kinyume na taratibu ndiyo haitakiwi, jambo ambalo linaweza kusababisha baadhi yao kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wote waliotoa lugha za matusi kwa Spika Makinda na Naibu Ndugai watachukuliwa hatua za kisheria. Tutawatafuta kwa njia zote, hii itasaidia kuwa fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo ambao wanapewa namba kwa manufaa ya wananchi, lakini wanazitumia kinyume chake,” alionya Kashililah.

“Tutawasaka kwa kila hali, tutawabaini tu kwa kushirikiliana na idara mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Polisi ili wachukuliwe hatua kali.”
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa chama chake baada ya kutoa namba hizo kwa wananchi alisema; “Bunge halijatuuliza ila wakituuliza tutajibu.”

No comments:

Post a Comment