Friday, May 24, 2013

Prof Jay: Sitaki hata udiwani!

Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Joseph Haule (Profesa Jay) amesema amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kukisaidia chama katika changamoto za kuikomboa nchi.
Akizungumza na Mwananchi jana Profesa J alisema hajajiunga na Chadema ili kugombea ubunge mwaka 2015, isipokuwa kwa dhumuni la kutaka kuongeza nguvu katika chama hicho akiwa kama kijana.
“Kujiunga na siasa si dhambi na haina maana kwamba nina mpango wa kugombea jimbo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Sihitaji kugombea hata udiwani ila ni kwa dhumuni la kutaka kuongeza nguvu katika chama ili kuyafikia malengo,” alisema.
Alisema yeye ni mfuasi wa Chadema tangu mwaka 2005 na amekuwa karibu na chama kwa nyakati nyingi lakini kwa sasa ameamua kuingia rasmi katika chama kama chachu katika kuongeza harakati kwa vijana.
“Nimeingia ili nisaidie hiki chama kuikomboa Tanzania kwani kwa muda mrefu niliokaa katika chama hiki nimegundua kuwa wamedhamiria kumkomboa msanii, kijana wa kawaida na wakubwa kwa wadogo hivyo nadhani nipo sahihi katika uamuzi wangu.”
“Natambua mimi ni mwanamuziki, sawa nina mashabiki wengi lakini haina maana kwamba sina haki ya kuchagua chama ninachoona mimi kinanifaa, lakini siwezi kusita kufanya kazi sehemu yoyote au wakati wowote chama kikinitaka nifanye kwa wakati husika,” alisema Profesa J.
Profesa J juzi alijiunga rasmi na chama hicho baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema mjini Dodoma na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi akiwa sambamba na msanii mwingine wa hiphop Kulwa Kinega maarufu kama K wa Mapacha ambaye alikabidhiwa kadi hiyo na Mbunge wa Ubungo John Mnyika.

 Source:Mwananchi

Thursday, May 23, 2013

Kikwete akemea vikali vurugu Mtwara

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewaonya watu wanaosababisha uvunjifu wa amani nchini humo kuwa watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Onyo hilo linafuatia ghasia ambapo ofisi kadha, maduka na nyumba zimechomwa katika mkoa wa Mtwara ulioko kusini mashariki mwa Tanzania leo.
Akihutubia kupitia televisheni ya taifa, TBC1, Rais Kikwete amesema wale waliokamatwa na polisi wakati wa ghasia hizo watashitakiwa.
Ghasia hizo zilianza muda mfupi baada ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni. Akizungumzia madai ya waandamanaji hao, Rais Kikwete amesisitiza kuwa raslimali za nchi ni mali ya taifa zima.
Amesema mkoa wa Mtwara haujatelekezwa na kusema kwamba kuna mipango ya kutumia gesi hiyo kujenga viwanda vya mbolea na kutumia gesi hiyo asilia kuzalisha nishati ya umeme kwa mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma ili kuunganishwa katika gridi ya taifa.

Ofisi zachomwa

Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa mkoa wa Mtwara kamanda Linus Sinzumwa, vurugu hizo zimetokea asubuhi ya leo mara baada ya Wizara ya Madini na Nishati kusoma bajeti yake ya makadirio ya mapato na matumizi huko Bungeni mjini Dodoma na kusababisha uharibifu wa mali.
Ametaja uharibifu huo kuwa ni pamoja na kuchomwa kwa majengo ya serikali kama mahakama, nyumba za watendaji wa serikali, baadhi ya majengo ya chama tawala na nyumba za watu binafsi.
Polisi wawasaka waandamanaji Mtwara
Hata hivyo, kamanda huyo, amekanusha taarifa za kuuawa kwa mtu mmoja katika eneo hilo na kubomolewa kwa daraja linalounganisha mji wa Mtwara na maeneo mengine.
Kamanda Sinzumwa amesema watu wapatao tisini na mmoja wanashikiliwa na jeshi na polisi kuhusiana na matukio mbalimbali ya ghasia hizo.
Ghasia hizo, zinahusishwa na madai ya muda mrefu sasa ya wananchi wa mkoa huo kupinga ujenzi wa bomba la gesi iliyogunduliwa mkoani humo kusafirishwa hadi Dar es Salaam, kaskazini mwa Mkoa wa Mtwara, kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme.
Hii ni mara ya pili mkoani Mtwara kutokea kwa ghasia zinazohusisha maafa kwa binadamu na uharibifu wa mali kama ilivyotokea mapem

Wednesday, May 22, 2013

PROFESA JAY AJIUNGA NA CHADEMA TAYARI KWA KUENDELEZA MAPAMBANO YA KISIASA KAMA MKONGWE SUGU

Rapper mkongwe nchini, Joseph Haule aka Profesa Jay amejiunga rasmi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA.
Profesa amekabidhiwa kadi ya uanachama wa CHADEMA na mbunge wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi aka Sugu. 
Kujiunga rasmi kwa Profesa kwenye chama hicho kunaashiria kuwa huenda akawa na nia ya kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho mwaka 2015.
 

Tuesday, May 21, 2013

Dragon boy

John Kerry kuzuru mashariki ya kati na Afrika



Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry anatarajiwa kusafiri kwenda katika mataifa ya mashariki ya kati na Afrika kuanzia Jumanne ijayo kwa ziara itakayomchukua hadi Mei 27.
Kerry  anatarajiwa  kuanza ziara  yake  mjini  Muscat  siku ya  Jumanne (21.05.2013), ikifuatiwa  na  Jordan  siku  ya  Jumatano, ambako atakutana  na  kile  kinachoitwa  "washirika  muhimu  wa  kimataifa", kuangalia uwezekano  wa  kupatikana  kwa  suluhisho  la  kisiasa kupitia  majadiliano  nchini  Syria , wizara  ya  mambo  ya  kigeni nchini  Marekani  imesema  katika  taarifa.
Mkutano  huo  unakuja  kabla  ya  mkutano  mkubwa  wa  kimataifa kuhusu  Syria unaopangwa  na  Urusi  na  Marekani , na  ambao unatarajiwa  kufanyika  mwezi  ujao.
Kerry akiwa katika majadiliano na rais Putin wa Urusi
Siku  ya  Alhamis  na  Ijumaa , Kerry anatarajiwa  kuzuru  Jerusalem na  Ramallah  kufuatilia  mazungumzo  juu  ya  kuleta  pamoja  Israel na  Palestina  katika  meza  ya  majadiliano, kujadili amani, taarifa hiyo  imesema.


Pia  siku  ya  Ijumaa , Kerry  anatarajiwa  kusafiri  kwenda  mjini Addis Ababa kushiriki  katika  sherehe  za  siku  mbili  za kuadhimisha  miaka  50  tangu  kuundwa  kwa  Umoja  wa  nchi  za Afrika  OAU, ambao  hivi  sasa   unajulikana  kama  Umoja  wa Afrika, AU. viongozi  kutoka  sehemu  mbali  mbali  za  Afrika watahudhuria  sherehe  hizo.
Hapo  Mei 26 , waziri  Kerry  anapanga  kurejea  mjini  Amman Jordan  kushiriki  katika  jukwaa  la  kiuchumi  la    dunia.
Wakati  huo huo  baraza  la  usalama  la  umoja  wa  mataifa  linatafakari ombi kutoka  kwa  maafisa  wa  ngazi  ya  juu  wa  shirika  la  misaada  la umoja  huo  linalodai  kufikishwa  kwa  misaada  katika  nchi iliyoharibiwa  kwa  vita  ya  syria, hatua  ambayo  inaweza kusababisha  hali  ya  mivutano  baina  ya  Urusi  na  mataifa  ya magharibi  kuhusiana  na  upelekaji  wa  misaada  ya  kiutu  kupitia mipakani, wamesema  wanadiplomasia  wa  Umoja  wa  Mataifa.

Monday, May 20, 2013

NGASSA ASAINI MKATABA WA IAKA MIWILI YANGA KATIKA PICHA





Source:salehjembe.blogspot.com

Assad asisitiza hatajiuzulu

Rais wa Syria Bashir al Assad
 

Rais wa Syria Bashar al Assad amesisitiza kuwa hatajiuzulu kabla ya mwisho wa kipindi chake madaraka mwaka 2014, wakati bomu lililotegwa katika gari liua watu watatu katika mji mkuu Damascus.
"Kujiuzulu ni sawa na kukimbia", Assad amesema katika mahojiano na gazeti moja la Argentina la Clarin wakati alipoulizwa iwapo anaweza kufikiria kujiuzulu kama waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry anavyotaka.
"Sifahamu iwapo Kerry ama yeyote mwingine amepata madaraka ya watu wa Syria kuzungumzia kwa niaba yao juu ya nani anapaswa kuondoka madarakani na nani anapaswa kubaki. Suala hilo litaamuliwa na watu wa Syria katika uchaguzi wa rais mwaka 2014.

Wanne wafa kwenye msongamano kanisani


Waumini kanisani Afrika Magharibi
Watu wanne wamekufa na 13 kujeruhiwa katika mkanyagano ndani ya kanisa la kiavengalisti nchini Ghana.
Ajali hiyo ilitokea pale waumini walipoania kufikia maji matakatifu katika tawi la kanisa la Synagogue Church of All Nations (SCOAN) katika mji mkuu, Accra.
Ripoti zinasema maelfu ya watu walikuwa wamekwenda kanisani humo.
Kanisa hilo liloanzishwa na kasisi wa Nigeria, TB Joshua, ambaye anasema yeye ni mtume.
Pia amezusha utata kwa kudai kuwa anaweza kutibu magonjwa yasiyotibika kama HIV na UKIMWI.

Chuji atwaa tuzo ya SuperSport ya mchezaji bora wa mechi


Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi ya kituo cha SuperSport katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba iliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Chuji alionyesha kiwango cha juu katika mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki 57,406 kwa kuiunganisha vyema safu ya kiungo ya Yanga.
Baada ya mechi hiyo kituo cha SuperSport kilichoonyesha mechi hiyo moja kwa moja kilimtangaza Chuji kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kuwafunika Didier Kavumbagu na Hamisi Kiiza wafungaji wa mabao ya Yanga.
Chuji alisema tuzo hiyo ameipokea kama changamoto kubwa kwake katika kuhakikisha anaendelea kucheza kwa kiwango cha juu siku zote.
“Nimefurahi kusikia hivyo sababu SuperSport ni watu wa mpira na watakuwa wameona uwezo wangu katika mechi hii, lakini hali hiyo naichukua kama moja ya changamoto kwangu,” alisema Chuji. Yaliyostaajabisha kipute cha watani wa jadi kama kawaida ya mtanange wa watani wa jadi yaani  Simba na Yanga huwa haukosi  matukio mageni ambayo huacha simulizi kwa mashabiki.
Haya ni baadhi tu matukio yaliyojiri kwenye mchezo huo uliopigwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwamuzi aanguka, mpira wasimama
Mashabiki wa soka walipigwa na “bumbuwazi” baada ya mwamuzi Martin Saanya aliyekuwa anachezesha mpambano huu wa Simba na Yanga kulala chini ghafla.
Tukio hili ambalo ni nadra kutokea kwenye viwanja  vya soka lilisababisha mpira kusimama kwa muda mrefu, ingawa ilikuja kubainika kwamba alipigwa kiwiko wakati akisuluhisha ugomvi baina na beki Said Nasoro ‘Cholo’ wa Simba na mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu.

Gari la ofisa mwandamizi wa Polisi Arusha lakamatwa likiwa na magunia 18 ya bangi

Gari aina ya Toyota Landcruiser linalotumiwa na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, lilikamatwa juzi mjini Moshi likiwa limesheheni magunia 18 ya bangi.
Habari za awali zilieleza kuwa gari hilo lilikamatwa juzi saa 4:00 usiku katika Mji mdogo wa Himo, Moshi Vijijini likisafirisha bangi hiyo kwenda Tarakea, Rombo.
Polisi wawili akiwamo dereva wa gari hilo wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Himo na gari lipo Makao Makuu ya FFU, Moshi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa askari hao: “Mchakato wa kuwafikisha mahakama ya kijeshi unaandaliwa. Bangi hiyo ilikuwa inapelekwa kwa mfanyabiashara mmoja huko Rombo na ndiye aliyewakodi.”
Hata hivyo, Kamanda Boaz alisema atatoa taarifa zaidi leo kwani uchunguzi bado unaendelea.
Bangi ilivyonaswa
Habari zimeeleza kuwa polisi waliokuwa doria waliliona gari hilo likitengenezwa na waliamua kuwauliza wenzao kulikoni? Wakajibiwa kuwa kuna kitu walikuwa wakirekebisha na lilikuwa ni tatizo dogo tu.
“Walipoulizwa kwani mnaelekea wapi wakasema wanapeleka mzigo wa bosi huko Tarakea mpakani na kwa taratibu zetu za kijeshi huwezi kuuliza ni bosi gani,” kilidokeza chanzo kimoja ndani ya polisi.
Hata hivyo, polisi hao wa doria walirudi katika gari yao ili waendelee na doria lakini baadhi ya polisi wakamweleza ofisa aliyekuwapo katika gari hilo kwamba wanashuku gari lile limebeba bangi.
“Lilikuwa na harufu kali ya bangi na hilo ndilo lililowafanya wale polisi kurudi tena kwa wenzao na kuwaambia wanataka waone wamebeba nini ndipo wakakutana na magunia 18 ya bangi,” 
Inadaiwa kuwa baada ya kukuta bangi hiyo, polisi hao waliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi (RCO), Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi ambaye naye alimjulisha Kamanda Boaz.
Ilielezwa kuwa Kamanda Boaz aliagiza kuwekwa mahabusu kwa polisi hao katika Kituo cha Himo na gari hilo lipelekwe FFU, Moshi.


Source:Mwananchi

Mchungaji Peter Msigwa wa CHADEMA akamatwa na Jeshi la Polisi.

Taaarifa kutoka Iringa zinasema mbunge wa Jimbo la Iringa Peter Msigwa wa CHADEMA amekamatwa na jeshi la polisi muda huu na yuko chini ya Ulinzi wa jeshi hilo.
Mchungaji Msigwa amekamatwa kwa amri ya Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Michael Kamuhanda kwa madai kwamba anawaunga mkono wafanyabiashara ndogondogo wa manispaa hiyo Machinga wanaopambana na polisi wanaowakataza kufanya biashara mjini.

Mchungaji Msigwa amekuwa mtetezi mkubwa wa wafanyabiashara ndogondogo kiasi kwamba kila anapoonekana maeneo ya manispaa hiyo hujikuta gari yake ikisukumwa na Machinga hao.

Itakumbukwa ni wiki iliyopita tu mbunge wa viti maalum Chadema Chiku Abwao alimshambulia vikali Waziri William Lukuvi kwamba analitumia jeshi la polisi Iringa kukandamiza Chadema na viongozi wake.

Mchungaji Msigwa ambaye pia ni mbunge machachari wiki iliyopita ametishiwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana kufikishwa mahakamani kwamba amemtuhumu kufanya biashara haramu ya pembe za ndovu.

Gari la Mbunge Mch.Msigwa kabla ya kukamatwa

Polisi wakitoka kumkamata Mch.Msigwa

Monday, May 6, 2013

Bomu Arusha:raia wa Saudia wanne wakatwa

Polisi nchini Tanzania inawashikilia watu wa nane kwa madai ya kuhusika na mlipuko wa siku ya jumapili katika kanisa Katoliki la Olasit viungani mwa mji wa Arusha.
Miongoni mwa washukiwa ambao wako mikononi mwa polisi ni raia wanne wa Saudi Arabia, na wengine wanne ni raia wa Tanzania.
Idadi ya watu waliofari dunia kufuatia mlipuko huo ni wawili na wala sio watatu kama ilivyoripotiwa hapo awali.
Polisi mjini Arusha vile vile wamethibitisha kuwa waliokufa wakati wa tukio hilo la kigaidi ni wawili.
Kwa wakati huu polisi wanachunguza ni kulipuzi aina gani kilitumika wakati wa shambulizi hilo.
Lakini Baruan Muhuza ambaye alitembelea eneo la tukio mbali na majeruhi hakuna hasara kubwa iliyotokea mahali hapo pia sakafi na kuta za kanisa hilo hazikuchimbika sana.
Watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia katika mlipuko huo uliotokea majira ya saa tano asubuhi katika kanisa katoliki la Olasit nje kidogo ya mji wa Arusha nchini Tanzania na wengine kadhaa kujeruhiwa huku balozi wa papa na watawa waliokuwa katika shughuli hiyo maalumu ya uzinduzi wa parokia mpya ya mtakatifu Yosefu mfanyakazi wakinusurika pia .
Kwa mjibu wa Padri Festus Mangwangi ambaye ni paroko msaidizi wa kanisa katoliki jimbo la Arusha mlipuko huo unapotokea walikuwa tayari katika hatua ya kubariki maji kwaajili ya uzinduzi wa kanisa ulikuwa ukiongozwa na balozi wa Papa Fransis.
Hata hivyo Padre Mangwangi amesema kuwa taarifa walizonazo muda mfupi baada ya majeruhi kukimbizwa hospitali watu kati yao wamefariki huku wengine wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mount Meru mjini Arrusha.
Shughuli zote kuhusiana na ibada hiyo zimesitishwa huku watalaalamu wa milipuko na polisi wakiendelea na uchunguzi kuhusiana na mlipuko huo.
Bado hakuna taarifa zozote kuhusiana na chanzo halisi cha bomu hilo ama kundi lolote linalodaiwa kuhusika na utegaji wa bomu hilo.
Hili ni shambaulio la kwanza la bomu nchini Tanzania japo kuwa mwaka huu pia kulikuwa na mtukio ya mauaji ya Padre wa kanisa hilo visiwani Zanzibar ambaye alipigwa risasi wakati akiwa anajiandaa kuingia kanisani.

Friday, May 3, 2013

SERIKALI YAFUTA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012

Serikali imetangaza kuanzia leo kufuta rasmi matokeo yote ya kidato cha nne mwaka 2012 na mitihani yote itasahihishwa upya kwa kutumia utaratibu ule uliotumika katika matokeo ya mwaka 2011.
Akisoma  bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu ripoti ya awali ya Tume ya kuchunguza kushuka kwa matokeo  ,waziri wa Uratibu na Bunge Williamu Lukuvi amesema hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Baraza la Mawaziri ambao waliopokea taarifa ya tume hiyo ambayo imependekeza hatua hiyo.


Kwa mujibu wa Tume hiyo, imependekeza mtihani wa kidato cha nne kusahihishwa upya huku ikiyafuta yale yaliyotangazwa kwa ajili ya kuweka usahihi na njia ya kuelekea kilele cha ubora wa elimu ya Watanzania wote.

Akizungumza Bungeni leo mjini Dodoma, Lukuvi alisema kuwa mitihani hiyo inapaswa kusahihishwa kwa kufuata kanuni ya mwaka 2011, hivyo uamuzi huo umetolewa na Tume ya Waziri Mkuu Pinda aliyounda baada ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutangaza matokeo ya kidato cha nne huku asilimia 60 ya wanafunzi wote kufeli.

Suala hilo liliibua mtafaruku mkubwa kwa wadau na wanasiasa wa Tanzania, wakililia haki ya mtoto wa Tanzania kusoma, huku wakisema kufeli kwao kutaongeza joto la maisha magumu kwa watoto hao ambao wengi wanatoka kwenye familia masikini.

Taarifa zaidi ya Tume hiyo na uamuzi wako itaendelea kukujia katika blog yako hii, kwa ajili ya kukufikishia habari kamili na namna ya kuwapatia haki ya kupata elimu watoto wa Tanzania.

Kijiwe Ughaibuni-18

Kijiwe 18 from Luke Joe on Vimeo.

KUFA AZIMIO LA ARUSHA:Nyerere alivyotofautiana na Mwinyi

Kumekuwa na mjadala kuhusu sababu za kufa kwa Azmio la Arusha. Azimio hilo lilianzishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama cha Tanu kikiwa na lengo la kutilia mkazo imani na siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea.
Halmashauri hiyo iliyokutana mjini Arusha Januari 26 - 29, 1967, ilijadili maadili ya viongozi wa umma, Serikali na vyombo vingine, pamoja na wanachama wa Tanu.
Katika maadili ya viongozi wa umma, iliamuliwa kuwa kiongozi wa Tanu (baadaye CCM) au wa Serikali, sharti awe ama mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au kikabaila.
Hata hivyo baada ya Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa anasimamia maadili hayo kung’atuka madarakani, misimamo hiyo ilianza kuyeyuka na kupigiliwa msumari wa mwisho huko Zanzibar.
Maamuzi ya Zanzibar
Mwaka 1991 Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi  (CCM) ilikutana mjini Zanzibar na kufanya mabadiliko ya azimio hilo.
Akizungumza na wazee wa chama, viongozi wa Taifa, mashirika ya umma na watu binafsi Februari 25, 1991 jijini Dar es Salaam, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM  hicho na Rais Ally Hassan Mwinyi aliwatoa hofu wale wanaodhani kuwa azio la Arusha linageuzwa.
“Inaelekea kuna hofu kwamba Azimio la Arusha linageuzwa. Kwa hiyo tangu mwanzo, kabla ya kusema lolote, nataka tuelewane kwamba siasa yetu bado ni ile ile ya Ujamaa na Kujitegemea,” anasema na kuongeza:
“Halikugeuka wala hatutazamamii kuligeuza. Kwa hali yoyote sisi wanachama wa Chama cha Mapinduzi hatutaweza kuigeuza siasa hii. Kule Zanzibar tulizungumza mengi, miongoni mwao ni kutoa tafsiri ya baadhi ya vipengele vya Azimio ili vifanane na wakati tulionao.”
Akifafanua zaidi, Mwinyi anasema tangu azimio hilo lilipoanzishwa mwaka 1967 hadi mwaka 1991 ilikuwa imepita zaidi ya miaka 20, hivyo kulikuwa na mabadiliko mengi duniani.
“Hali yetu ya sasa hasa ya kiuchumi, siyo ile ya mwaka 1967. Ndiyo maana mishahara ya wafanyakazi ingawa imeongezeka sana, lakini bado haikidhi mahitaji yao, haiwatoshi hata wale wanaopokea mishahara mikubwa miongoni mwetu,” anasema na kuongeza:
“Isitoshe, wakati wa Azimio idadi ya Watanzania ilikuwa ndogo, sasa hivi idadi yetu imeongezeka zaidi ya mara mbili . Kwa sababu ya wingi wetu, mahitaji yameongezeka sana, wakati mapato yetu yamekuwa yakipungua wakati wote.”
Mwinyi anaongeza kuwa kila zama na mwongozo wake:
“Msahafu wa Waislamu unasema “Likulli ajalin kitab’, yaani kila zama ina kitabu chake,” anasema na kuongeza:
“Sisi wana CCM tunakubali kuwa kila zama zinahitaji kuwa na mwongozo wake. Azimio la Arusha ni mwongozo wetu wa msingi. Ni dira inayoongoza mwelekeo wa jamii yetu. Lakini tafsiri zake inabidi zirekebishwe kila inapohitajika ili zisipitwe na wakati.”
Akisisitiza kuhusu ufafanuzi wa maamuzi ya Zanzibar anasema baada ya kutangazwa kwa azimio la Arusha mwaka 1967 lilifuatiwa na matamko kama vile Azimio la Iringa la mwaka 1971 la ‘Siasa ni Kilimo’ na mwongozo wa mwaka 1981 uliotolewa kwa lengo la kukuza tafsiri ya Azimio la Arusha.
Anaongeza kuwa hata mwaka 1974 kulikuwa na agizo la Musoma kuhusu Elimu ya Kujitegemea.
“Maandiko hayo yote hayakupingana na Azimio la Arusha, ila yaliongeza mambo ambayo yalihitajika yafanane na wakati wake,” anasema.
Akizungumzia sababu ya kuanzishwa kwa Azimio la Arusha mara baada ya nchi kupata uhuru, anasema baadhi ya viongozi walianza kutumia uongozi wao kama mradi wa kujineemesha.
Msimamo wa Nyerere
Licha ya Rais wa awamu ya pili kufafanua umuhimu wa uamuzi wa Zanzibar, bado Mwalimu Nyerere aliendelea kutoridhika kuhusu msimamo mpya wa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari mwaka 1999, Mwalimu Nyerere alisema bado alikuwa hajaona kasoro ya Azimio la Arusha. “Mimi bado natembea nalo (Azimio la Arusha). Nalisoma tena na tena kugundua kama kuna cha kubadili. Labda ningeboresha Kiswahili nilichokitumia, lakini Azimio lenyewe bado ni thabiti. Nisingebadili hata neno moja,” anasema Mwalimu Nyerere.

Source:Mwananchi

260,000 WALIKUFA KWA UKAME SOMALIA

Watoto wengi walikufa kwa Utapia mlo
Takriban watu 260,000 walifariki dunia wakati wa ukame ulioikumba Somalia kuanzia mwaka 2010 hadi 2012, utafiti umebaini.
Nusu ya waliofariki dunia walikuwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, inaeleza ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, pamoja Mtandao wa Kuonya Mapema Kuhusu Majanga ya Ukame unaofadhiliwa na Marekani.
Idadi ya vifo ilikuwa kubwa kuliko ile iliyokadiriwa ya watu 220,000 waliofariki wakati wa ukame wa mwaka 1992.
Janga hilo lilisababishwa na ukame mkali, uliochochewa na mapigano kati ya makundi hasimu yaliyokuwa yakigombea madaraka.
Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ulitangaza hali ya ukame Julai 2011 katika mikoa ya Somalia ya Bakool uliopo kusini na ule wa chini wa Shabelle, ambayo ilikuwa inadhibitiwa na kundi la wanamgambo wa Al – Shabab wenye mafungamano na Al – Qaeda.
Lakini kundi hilo lilikanusha kuwepo kwa hali hiyo na kuyapiga marufuku mashirika kadhaa ya misaada ya nchi za magharibi kufanya shughuli zake katika maeneo hayo.
Baadaye ukame ulisambaa katika maeneo mengine ukiwemo mkoa wa kati wa Shabelle na Afgoye na katika kambi za watu wasiokuwa na makaazi katika maeneo yaliyokuwa yakidibitiwa na serikali katika mji mkuu Mogadishu.
Mchumi Mwandamizi wa shirika la FAO, Mark Smulders amesema, ukweli kuhusu ukubwa wa janga hilo la kibinadamu umeibuka kwenye utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Mtandao wa Kuonya Mapema Majanga ya Ukame, Fews Net.
“Kwa kawaida, kukadiria vifo wakati wa dharura ni sayansi isiyo rasmi, lakini kutokana na ubora na kiwango cha takwimu zilizokuwepo, tuna uhakika na utafiti huo”, amesema ofisa wa Fews Net Chris Hillbruner.
“Utafiti huo unaeleza kuwa, kilichotokea Somalia ni moja ya majanga mabaya kabisa ya ukame kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, “ ameongeza.
Inakadiriwa kuwa 4.6% ya jumla ya idadi ya watu na 10% ya watoto chini ya umri wa miaka mitano walifariki dunia huko maeneo ya kusini na kati mwa Somalia, imeeleza ripoti hiyo.
“Ripoti hiyo imethibitisha kuwa hatua za ziada zingechukuliwa kabla ya ukame huo haujatangazwa, amesema Phillippe Lazzarini, Mratibu wa Shughuli za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Somalia ilikumbwa na ukame mkali mwaka 2011, ulioathiri zaidi ya watu milioni 13 katika eneo lote la Pembe ya Afrika.
Maelfu ya watu walikimbia makaazi yao wakisaka chakula. Umoja wa mataifa ulitangaza ukame huo kumalizika Februari 2012.
Kwa zaidi ya miaka 20 ya vita vya weyewe kwa wenyewe, Somalia imeshuhudia wababe wa kivita wa koo, wanasiasa mahasimu na vikundi vya wanamgambo vikigombea madaraka, hali iliyoruhusu kushamiri kwa ukosefu wa utawala wa sheria.
Septemba mwaka jana, serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliingia madarakani baada ya miaka nane ya utawala wa mpito, hatua iliyoleta utengamano katika baadhi ya maeneo.