Friday, June 28, 2013

Familia ya Mandela yakosoa wanahabari

Mabango ya kumtia moyo Mandela
Taarifa kutoka Ikulu ya Afrika Kusini zinasema kuwa hali ya kiafya ya rais mstaafu Nelson Mandela sio nzuri na kuwa imezorota katika saa 48 zilizopita.
Baada ya kumtembelea hospitalini, mwanawe mkubwa wa kike Makaziwa, alisema hali inaonekana kuwa mbaya lakini akaongeza kuwa Mandela anaweza kuwasikia jamaa zake wanapomuita huku akijaribu kufungua macho yake.

Wamevuka mipaka ya maadili. Wakati hayati Margaret Thatcher alipokuwa mgonjwa mbona sikuona, ukaribu wa vyombo vya habari kiasi ninachokiona kwa banangu? Ni kwa sababu hii ni nchi ya kiafrika. wanahisi kuwa hapa wanaweza kuvuka mipaka wanavyotaka, '' alisema MakaziweMakaziwe amesema “Nimekasirishwa sana. Kwa sababu Mandela ni kiongozi mashuhuri duniani, haimaanishi utu wake udhalilishwe pamoja na kuvuka mipaka kuingilia mambo yake binafsi Hapa naona kuna ubaguzi wa rangi, huku vyombo vingi vya kimataifa vikivuka mipaka, ni kama ndega aina ya Tai au Vulture wanaosubiri Simba kumla mnyama aliomuwinda kisha wakimbilie mzoga.
Mapema leo, Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma alifutilia mbali ziara yake ya kwenda Musumbiji baada ya kumtembelea hospitalini aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Rais Zuma amesema kuwa Bwana Mandela yuko katika hali mbali ya afya.
Msemaji wa Zuma Mac Maharaj alisema kuwa hali yake imedorora zaidi
Mandela ambaye, ni rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, amelazwa hospitalini tangu tarehe 8 mwezi Juni akiugua maradhi ya mapafu.
Madaktari wanasemekana kufanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa Mandela anapona.
Vikundi vya watu wenye huzuni mkubwa kuhusu hali ya afya ya Mandela, walikusanyika nje ya hospitali alikolazwa, wakiwa na ujumbe wa ugua pole kwa Mandela
Wadadisi wanasema kuwa wananchi wa Afrika Kusini wanaonekana kuwa tayari kwa habari zozote sasa kuhusu hali ya Mandela.
"tutasikitika sana ikiwa tutapata habari za kifo chake, lakini pia tutakuwa tunasherehekea maisha yake. Amefanya mambo mengi zaidi kwa nchi yetu,'' alisema kijana John Ndlovu, mwenye umri wa miaka 25.
Zuma alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa marais nchini Msumbiji, hii leo lakini akaamua kuakhirisha safari yake.
Taarifa kutoka kwa ofisi yake ilisema kuwa anaendelea kuwapongeza wananchi wa Afrika Kusini wanaoendelea kuiombea familia ya Madiba.
Uamuzi wa Rais Zuma kufutilia mbali ziara yake ambako alitarajiwa kuhudhuria mkutano wa kikanda kuhusu uekezaji anaonyesha wazi kuwa hali ya Mandela inaendelea kuzorota zaidi 

Rais Morsi aonya dhidi ya maandamano

Rais wa Misri Mohammed Morsi ameonya kuwa vurugu za siasa zinaathiri demokrasia nchini humo.

Katika hotuba ya taifa kupitia televisheni kuadhimisha mwaka mmoja tangu achukue uongozi, Bw Morsi alikiri kuwa amefanya makosa kadhaa.

Hata hivyo uongozi wake umekumbwa na changamoto si haba ambapo Misri imeshuhudia maandamano ya kila mara kati ya wafuasi na wapinzani wa Morsi.Kadhalika aliutaka upinzani kuwasilisha matakwa yake kupitia kura.
Morsi pia amewonya wale wanaonekana kama wenye njama ya kutaabisha utawala wake na kujairbu kumwendea kichinichini pamoja na kusumbua demokrasia nchini humo.
Wanajeshi wamepelekwa katika miji mikubwa kote nchini kabla ya kufanyika kwa maandamano yanayopangwa dhidi ya utawala wake mwishoni mwa wiki hii.
Hotuba ya bwana Morsi imetolewa wakati makabiliano yakitokea Kaskazini mwa mji wa Mansoura.
Watu wawili waliuawa na wengine 170 kujeruhiwa kwenye mapigano kati ya wafuasi na wapinzani wa serikali, kwa mujibu wa afisaa wa afya.
Morsi anayeongoza chama tawala cha Muslim Brotherhood, alikuwa rais wa kwanza wa taifa hilo kwa chama cha kiisilamu babada ya kushinda uchaguzi mwezi Juni mwaka jana.
Uchaguzi huo ulisifiwa na wengi kuwa huru na wa haki. Mwaka wake wa kwanza mamlakani umekumbwa na maandamano ambayo hayaishi pamoja na uchumi unaodorora.

Chadema wamjibu Waziri Mkuu

Dodoma. Chama cha Maendeleo, Chadema kimeibuka jana bungeni na kusema Serikali inafahamu ukweli wa mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa chama hicho jijini Arusha.
Chama hicho kimesema Serikali ilitumia kutokuwepo kwao bungeni kupotosha wananchi kuhusu hali halisi juu ya mlipuko wa bomu hilo uliotokea wakati chama hicho kikihitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika Viwanja vya Soweto jijini Arusha, Juni 15, mwaka huu.
Akizungumza kabla ya kuanza kuchangia muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2013/2014, Waziri kivuli wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi wa Chadema, Halima Mdee alisema, “Kabla sijaanza kuchangia Mheshimiwa Spika naomba nianze kwa kuwapa pole wakazi wote wa Arusha kutokana na mlipuko wa bomu uliosababisha watu kupoteza maisha, kwani tangu limetokea tukio hilo leo ndiyo nazungumza kwa mara ya kwanza,”
“Tunazilaani kauli potofu zilizotolewa na Serikali hapa bungeni, Serikali inajua nini kilichotokea Arusha na ilitumia kutokuwepo kwetu kupotosha,” alisema.
Source:Mwananchi

Tuesday, June 25, 2013

Hali ya wasiwasi kuhusu afya ya Mandela


Wananchi wa Afrika Kusini hii leo wamekuwa na wasiwasi baada ya rais wa nchi hiyo Jacob Zuma kutangaza kuwa hali ya afya ya rais mstaafu Nelson Mandela sio nzuri sana.
Asubuhi waliamkia kwenda kazini wasijue taarifa watakazopokea hii leo baada ya rais Zuma kutoa taarifa hiyo.
Afisaa mmoja mkuu alisema kuwa raia wa Afrika Kusini wasiwe na matumaini kupita kiasi.Taarifa kutoka ikulu ya rais zilisema Jumapili jioni kuwa Mandela alikuwa amezidiwa ingawa madaktari wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa anapata afueni.
Mandela ambaye alikuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, akiwa na umri wa miaka 94,alipelekwa hospitalini mapema mwezi huu, ikiwa ni mara ya tatu kwake kulazwa hospitalini akiugua ugonjwa wa mapafu mwaka huu.
Rais Jacob Zuma alisema Jumapili kuwa alimzuru Mandela Hospitalini na kuzungumza na mkewe kuhusu hali ya rais mstaafu.
Madaktari wanaomtibu Mzee Nelson Mandela wamesema hali yake imekuwa sio nzuri kwa saa ishirini na nne zilizopita na sasa ni mahututi.
Habari hizo zimekuja kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais ya Afrika Kusini.
Taarifa hiyo imesema bado Mzee Mandela ameendelea kusalia hospitalini mjini Pretoria kwa siku ya kumi na sita akitibiwa mapafu yaliyosababisha tatizo kwenye mfumo wake wa upumuaji.
Rais Jacob Zuma amemtembelea Mzee Mandela na pia kuzungumza na jopo la matabibu wanaomtibu.
Baadaye bwana Zuma alirejea kauli yake ya kulitaka taifa na dunia kumuombea Mzee Mandela apate nafuu.

Wamarekani wamwalika Kabwe Zitto


Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Kaskazini(Chadema), Zitto Kabwe amealikwa kuhudhuria tamasha la tisa la Aspen mwaka huu, linaliofanyika Marekani.
Tamasha hilo linawajumuisha pamoja watu mashuhuri katika nyanja mbalimbali duniani lengo likiwa ni kuwawezesha kubadilishana mawazo na uzoefu.
Kwa mujibu wa taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto amesema ushiriki wake katika tamasha hilo utamwezesha kukutana na kubadilishana mawazo na magwiji wa masuala mbalimbali duniani.
“Nimefurahi kupata mwaliko huu na nimekubali kushiriki kwa sababu kwangu mimi hii ni nafasi adhimu sana na kupanua uelewa wangu wa masuala mbalimbali, pia ni fursa kubwa ya kueleza maoni yangu kwa waalikwa wenzangu. Nina uhakika kuwa watu nitakaokutana na kubadilishana nao mawazo na uzoefu watasaidia kupanua uelewa wangu wa masuala kadhaa,” alisema Zitto.
Alisema tamasha hilo litaendeshwa litaanza Juni 26 mwaka huu, limegawanyika katika sehemu mbili.
Alisema ya kwanza itahusisha majadiliano ya pamoja, ya vikundi na ya mtu mmoja mmoja.
Source:Mwananchi

Monday, June 24, 2013

Mshtakiwa wa EPA asimulia jinsi wajanja walivyomzidi ‘kete’ kwenye akaunti yake

Mkurugenzi wa Kampuni ya Principal Ltd, Godfrey Mosha amesimulia jinsi Benki ya Akiba Commercial (DCB), tawi la Kariakoo, ilivyoidhinisha malipo ya fedha kwa mtu mwingine kutoka akaunti yake ndani bila yeye kujua.
Mosha ni mmoja wa washtakiwa katika kesi ya  wizi wa fedha kwenye  Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Pamoja na wenzake, Bahati  Mahenge, Manase Makale, Davis Kamungu na Eda Makale, wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh1.86 bilioni za EPA, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuipitia Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex.
Katika kesi hiyo dhidi ya DCB, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Warialwande Lema, Mosha anaidai benki hiyo Sh46.8 milioni, zilizolipwa kwa mtu asiyemfahamu kwa kutumia hundi nne tofauti na tarehe tofautitofauti.
Katika ushahidi wake Ijumaa  iliyopita, akiongozwa na Wakili wake, Michael Ngalo, Mosha alidai  alibaini uhamisho huo wa fedha  kutoka  akaunti yake namba 0400438671, Novemba 15, 2011 alipochukua taarifa ya benki.
Alidai kuwa baada ya kubaini uhamisho huo, alikwenda makao makuu ya benki hiyo ambako alimuona Meneja wa Fedha, Vicent Anthony na kumweleza kuhusu tukio hilo wakati yeye hajawahi kuidhinisha uhamisho huo.
“Vicent aliniambia kuwa siyo transfer (uhamisho), bali ni malipo yaliyofanyika kwa kutumia cheque (hundi). Aliniambia namba za hundi hizo na ikaonekana kuwa zililipwa kwa Rafael John Mkwabi, mwenye namba ya akaunti 11000787541,” alidai Mosha na kuongeza:
“Huyo John sijawahi kumwandikia hundi, wala sijawahi kufanya naye biashara, sijawahi kukutanana naye, wala simfahamu.”
Mosha alidai kuwa hundi hizo zilikuwa zimesainiwa na Vicent na Meneja Mkuu, Salehe Ramadhan, huku akidai kuwa saini inayoonekana katika hundi hizo siyo yake.
Alizitaja hundi hizo kuwa ni hundi namba 083722, ya Sh11.6 milioni iliyolipwa Novemba 11, 2011 na  hundi namba 083723 ya Sh9 milioni, iliyolipwa tarehe hiyo.
Nyingine ni  hundi namba 083724 ya Sh14.4 milioni iliyolipwa Desemba 2011, hundi namba 083725 ya Sh11.8 milioni iliyolipwa Desemba 3, 2011.
Aliziwasilisha mahakamani hundi hizo na nyaraka mbalimbali zinazoonyesha saini yake halisi, mahakama ilizipokea kama vielelezo vya ushahidi.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Wakili Ngalo alifunga ushahidi na mahakama ilipanga kuendelea na usikilizaji kesi hiyo Julai 8, wadaiwa wataanza kujitetea.

Source:Mwananchi

Friday, June 21, 2013

Mabondia wa Tanzania wafungwa Mauritius

Mabondia waliohukumiwa


Mabondia wanne wa Tanzania wafungwa miaka 15 jela nchini Mauritius kwa makosa ya kuingiza dawa za kulevya aina ya heroin.

Mabondia hao ni Case Ramadhani Fills, Nathanael Elia Charles, Ally Rajabu Msengwa na Petro Charles Mtagwa.
Wakiwa mbele ya Jaji, waliiambia mahakama kuwa walilazimika kuingia katika biashara hiyo haramu kutokana na hali zao za maisha kuwa maskini.Wakati kesi hiyo ilipoanza kusikilizwa, wote walikiri makosa ya kuingiza mihadarati hiyo nchini Mauritius wakati walipokwenda kushiriki mashindano ya ndondi barani Afrika mwaka 2008.
"Tunaomba radhi kwa taifa la Mauritius", waliiambia mahakama.
"Tu watu maskini na tunategemewa na familia, watoto na wazee wetu wanatutegemea."
"Kwa dawa hizi tungepata kiasi cha Pauni £4,000". walisema
Jaji Benjamin Marie Joseph alisema katika kutoa adhabu hiyo yote hayo ameyafikiria, kwani walitoa ushirikiano mzuri wakati wote wa uchunguzi wa kesi hiyo, kulikowezesha hata wafanyabiashara hiyo, raia wa Mauritius kukamatwa.
Wamekuwa mahabusu kwa siku 1,722, sawa na miaka mitano, hivyo watatumikia miaka kumi iliyobakia jela. Pia watatakiwa kulipa faini ya pauni £1,600 na gharama nyingine za uendeshaji wa kesi hiyo.
Kwa mujibu chanzo cha habari nchini Mauritius, Jaji aliwashutumu kwa kuukosea umma wa Mauritius kwa kuingiza dawa hizo za kulevya aina ya heroin.
Mabondia hao waliwasili Mauritius tarehe 10 Juni 2008 na kuweza kupita uwanja wa ndege bila kunaswa hadi walipokamatwa katika hoteli waliyofikia ya Quatre Bornes.
Kwa pamoja walimeza gram 4639.04 za heroin zikiwa katika vifuko 358 vijulikavyo kama pipi.

Wabunge Chadema wasimulia mkong’oto

Mbunge wa Singida Mashariki,Tundu Lissu akiwaonyesha waandishi wa habari miwani yake aliyodai kuvunjiwa na polisi. Lissu alipata dhamana katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, jijini Arusha jana baada ya kukamatwa juzi. Picha na Moses Mashalla 





Arusha/Dar es Salaam. Wabunge wanne wa Chadema, ambao waliachiwa na polisi kwa dhamana wamesimulia mateso waliyoyapata wakiwa rumande baada ya kukamatwa juzi.
Vigogo hao; Mbunge wa Mpanda Mjini Said Amour Arfi, Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti maalumu), walikamatwa juzi baada ya wao na wafuasi wa chama hicho kutawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi kwenye Viwanja vya Soweto, Arusha.
Wabunge hao waliachiwa baada ya kujidhamini wenyewe huku watu wengine 65 waliokamatwa pamoja nao wakiachiwa baada ya kudhaminiwa.
Wote wanatakiwa kuripoti kwenye kituo hicho Julai 22, mwaka huu na wataelezwa hatma ya suala hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jeshi lake linaendelea kuwasaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema na kuwaonya kuwa wanatakiwa kujisalimisha mara moja.
Chagonja alisema Mbowe na Lema wanatafutwa kwa kosa la kufanya kusanyiko lisilo halali katika viwanja hivyo vya Soweto walipokuwa wakitaka kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki dunia baada ya kuumizwa kutokana na mlipuko wa bomu, Jumamosi iliyopita.
Pia aliwaamuru Mbowe na Lema kuwasilisha mara moja ushahidi wa kuwahusisha polisi na shambulio la bomu na kama hawana imani na Polisi, basi wawasilishe ushahidi wao kwa Rais Jakaya Kikwete.
Lissu
Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alilalamikia kitendo cha polisi kumwagia maji ya kuwasha baada ya kumkamata.
“Walinimwagia maji ya kuwasha kwa mfululizo nikalazimika kulala chini kifudifudi huku nikiwa nimefunika macho kukwepa yasiingie maji. “Kuna askari walitaka kunipiga lakini niliokolewa na mwenzao mmoja aliyenikinga nisishambuliwe. Kwa kweli ilikuwa hali ya hatari,” alisema.
Alisema polisi hao waliomkamata walivunja miwani yake kwa makusudi akisema aliikabidhi kaunta ikiwa haijavunjika.
“Wakati naingia mahabusu nilikabidhi miwani yangu lakini ajabu wakati tukiachiwa ilikuwa imevunjika.” Alilalamikia hatua ya polisi kuwashambulia kwa mabomu, kuwamwagia maji ya kuwasha walipokuwa wakiwatawanya watu waliokusanyika Soweto akisema awali, waliwaruhusu.

Wednesday, June 19, 2013

Polisi yataka ushahidi wa Mbowe, Lema na Nape

Arusha/Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetishia kuwakamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na limesema litamhoji Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye baada ya wanasiasa hao kudai kufahamu watu waliohusika na tukio la kurushwa bomu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja aliwataka wanasiasa hao kuwasilisha ushahidi wa kile wanachofahamu kuhusu kulipuliwa kwa bomu hilo.
Juzi, Mbowe akiwa na Lema, alisema wana ushahidi wa picha za video zikiwahusisha polisi na kulipuliwa kwa bomu hilo katika Uwanja wa Soweto wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani kwa Chadema, Jumamosi iliyopita.
Mkwara wa Chagonja
Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kupeleka ushahidi ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
“Tunamtaka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa askari wetu kuhusika na tukio la bomu pale Soweto. Wasipofanya hivyo tutatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo kwani yeyote mwenye ushahidi unaoweza kusaidia upelelezi wa kosa la jinai akikataa kuuwasilisha kwa vyombo husika anaweza kuchukuliwa hatua,” alisema.
Nape naye kuhojiwa
Kwa upande wake, polisi limesema litamhoji Nape ambaye alikaririwa jana akidai kuwa Chadema ndiyo waliohusika na urushaji wa bomu kwenye mkutano wao baada ya kuhisi kushindwa kwenye uchaguzi wa kata nne za Jiji la Arusha.
Kamishna Chagonja alisema watamhoji ili kusaidia kazi yao ya upelelezi. Nape aliihusisha Chadema kwa kauli alizoita za kutishia amani zilizowahi kutolewa siku za nyuma kabla ya uchaguzi wa kata za Arusha.
Watatu wakamatwa
Kamishna Chagonja alisema watu watatu wamekamatwa wakihusishwa na tukio la kulipuliwa kwa bomu mkoani Arusha.
Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi na watafikishwa mahakamani muda wowote ushahidi wa kutosha utakapopatikana au kuachiwa huru wakigundulika kutokuhusika.
Source:Mwananchi

Thursday, June 6, 2013

Uingereza kuwafidia Mau Mau Kenya

Serikali ya Uingereza inatarajiwa kuomba msamaha pamoja na kuwalipa fidia manusura wa harakati za ukombozi wa Uhuru wa Kenya Mau Mau.
Waliokuwa wanachama wa vuguvugu hilo waliwasilisha kesi mahakamani kwa mateso na dhuluma walizodai kutendewa na uliokuwa utawala wa ukoloni miaka ya 50.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague, anatarajiwa kutangaza kiwango cha pesa ambazo serikali ya Uingereza iko tayari kutoa kama fidia, duru zikisema kuwa huenda ikawa dola milioni 20
Zaidi ya wakenya 5,000, waliteswa baadhi wakinyanyaswa na waliokuwa wakoloni wa Uingereza.

Uingereza ilipigana vita vikali dhidi ya Mau Mau, waliokuwa wanadai ardhi na kuondoka kwa utawala wa kikoloni.
Manusura wa vita hivyo wamekuwa wakiidai Uingereza kuwalipa fidia kwa miaka mingi.
BBC ina habari kuwa bwana Hague atawaomba radhi waathiriwa wa vita vya Mau Mau, wakati akitangaza kiwango cha pesa watakazotoa kama fidia kwao.

Serikali ya Uingereza awali ilikuwa imesema kuwa madai yote ya vitedno walivyofanya wakoloni ni juu ya serikali ya Kenya tangu kuipa uhuru mwaka 1963 na kuwa kwa sasa haiwezi kutakiwa kulipa.
Lakini mwaka 2011, mahakama iliamuru kuwa, wanaodai fidia, Paulo Muoka Nzili, Wambuga Wa Nyingi na Jane Muthoni Mara, walikuwa na haki ya kudai fidia kutoka kwa Uingereza .

Mawakili wao wanasema kuwa Nzili alihasiwa , huku Bwana Nyingi akichapwa vibaya wakati Bi Mara akiteswa kimapenzi katika kambi za mateso ambako waliokuwa wanapinga ukoloni walikuwa wakifungwa.

Baada ya uamuzi wa kesi hiyo, ilirejeshwa katika mahakama kuu ili kuamua pesa watakazolipwa na ofisi ya jumuiya ya madola.
Habari zinasema kuwa serikali ilikumbwa na wakati mgumu kupata mashahidi na stakabadhi muhimu kuweza kuelezea ukweli katika kesi hiyo.
Lakini Oktoba mwaka jana, mahakama iliamua kuwa waathiriwa waliowasilisha kesi hiyo mahakamani walikuwa na haki ya kufidiwa kwani walikuwa na kesi nzito dhidi ya serikali ya Uingereza.

Watatu hao walikuwa wamesema kuwa wangekubali wahusika wa kesi kuafikiana nje ya mahakama lakini pia walikuwa wanataka kufuata sheria kwani waliona wangepata haki katika mahakama.

Vigogo wanne upinzani wafikishwa mahakamani vurugu za Mtwara

Viongozi wanne wa vyama vya upinzani mkoani Mtwara, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi, Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara.
Awali Katani, Uledi na Licheta walifikishwa mahakamani Mei 31 mbele ya Hakimu Mfawidhi Mwandamizi, Dainess Lyimo, kabla ya kuunganishwa na Kulaga ambaye alikamatwa Juni 2 mwaka huu na kufikishwa mahakamani peke yake Juni 3.
Hata hivyo, juzi washtakiwa wote wanne waliunganishwa na kufikishwa kwa Hakimu Mkazi Mussa Esanju, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa Hakimu Lyimo yupo safarini.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Justine Sanga, alidai washtakiwa hao kwa pamoja walikutana mahali na muda usiojulikana na kula njama hizo.
Sanga alidai shtaka la pili, Januari 16, mwaka huu eneo la Bima mjini Mtwara, washtakiwa kwa pamoja walidaiwa kufanya makosa ya uchochezi, kwa kutoa hotuba kwa wakazi hao, kwa lengo la kuleta chuki na kusababisha kuharibu mali za umma na binafsi.
Pia, alidai shtaka la tatu Januari 16, mwaka huu eneo la Bima washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuamsha hisia mbaya, kufanya mikutano ya kisiasa, kutoa maneno makali na kusababisha kuamsha hisia mbaya za wananchi.
Wakili wa utetezi, Banana Biboze aliomba mahakama kumwachia mteja wake, Hassan Uledi, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (Mum) kwa ajili ya maandalizi ya mitihani yake Juni 16, mwaka huu.
Hata hivyo, mahakama haitoa dhamana kwa washtakiwa hao kwa kile kilichodaiwa ni kwa ajili ya usalama wa washtakiwa na jamii na kwamba, Hakimu Lyimo anayesikiliza kesi hiyo yupo safarini.
Washtakiwa kwa pamoja walikana mashtaka na kurudishwa rumande hadi Juni 13, mwaka huu.

Source:Mwananchi