Saturday, April 4, 2015

Burundi : Spika wa bunge azuiliwa kusafiri

Joto la kisiasa limeendelea kupanda nchini Burundi kufuatia nia ya rais Pierre Nkurunziza ya kugombea muhula wa tatu, huku wafanyakazi wa serikali wanaopinga kugombea kwa Pierre Nkurunziza muhula wa tatu wakifutwa kazi.
Wakati huohuo, Spika wa Bunge nchini Burundi, Pie Ntavyohanyuma amezuiliwa Alhamisi wiki hii kusafiri kwenda nchini ubelgiji katika ziara ya kikazi. Wizara ya fedha imemuomba kiongozi huyo kutoa maelezo kuhusu matumizi ya Euro elfu thelathini aliyopewa alipofanya ziara ya kikazi nchini Kenya. Lakini wengi wanaona kwamba kuzuiliwa kwa Spika huyo, kunaambatana na malumbano yanayojiri wakati huu katika chama madarakani Cndd-Fdd.
Aliyekuwa kiongozi wa chama cha Cndd-Fdd, Hussein Radjabu ameikosoa nia ya rais Nkurunziza ya kutaka kugombea muhula watatu, akisema kwamba iwapo rais huyo atafanya hivyo atakua amewakosea wafuasi wa chama cha Cndd-Fdd pamoja na raia wa Burundi kwa ujumla.
Hayo yakijiri, wito uliyotolewa na mashirika ya kiraia wa kuwataka raia popote pale walipo kupiga honi, firimbi na kogonganisha vyuma saa sita mchana Alhamisi Aprili 2, umeitikiwa mjini Bujumbura na katika sehemu mbalimbali za nchi.
Jumatano wiki hii katika mkutano na waandishi wa habari kiongozi wa muungano wa mashirika ya kiraia Forsc, Vital Nshimirimana, amesema wito huo kwa raia ni kama kadi nyekundu anayopewa mchezaji wa soka aliyefanya madhambi, akibaini kwamba rais Nkurunziza atakua amepewa kadi nyekundu.
Hayo yanajiri wakati Kaskazini mwa nchi hiyo, hasa katika mkoa wa Kirundo zaidi ya raia 300 wamekimbilia nchi jirani ya Rwanda, wakisema wanahofia usalama wao kutokana na hali inayojiri wakati huu nchini mwao. Waziri wa Rwanda mwenye dhamana ya wakimbizi, Serafine Mukantabana amesema serikali yake imejenga kambi mbili ambapo watapewa hifadhi wakimbizi hao.
Waziri Mukantabana ameongeza kuwa wako mbioni kuwapatishia matibabu baadhi ya wakimbizi ambao wameanza kusumbuliwa na maradhi mbalimbali.


No comments:

Post a Comment