Saturday, May 16, 2015

TFF waigeuka kauli yao, sasa waibebesha msalaba CECAFA kuhusu Simba, Mbeya City

SHIRIKISHO la soka Tanzania, TFF, limeshindwa kuthibitisha moja kwa moja kama ni Simba au Mbeya City fc itakayoshiriki kombe la klabu bingwa Afrika mashariki na kati, maarufu kwa jina la ‘Kagame Cup’ linalotarajia kuanza kutimua vumbi Julai 11 hadi Agosti 2 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine ameuambia mtandao huu kuwa CECAFA ndio watakaosema ni timu gani ya tatu nchini Tanzania wameialika kushiriki Kagame.
Kauli hii inatofautiana na ile aliyowahi kusema kupitia mtandao huu kuwa TFF wameichagua Simba badala ya washindi wa tatu wa msimu  wa 2013/2014 wa ligi kuu soka Tanzania bara, Mbeya City fc.
“Kimsingi na kwa taratibu wawakilishi wa Tanzania ni bingwa wa msimu uliopita (2013/2014) ambao ni Azam na mshindi wa pili ambaye ni Yanga anayefaidika na uenyeji wa Tanzania”. Amesema Mwesigwa na kuongeza: “Lakini Cecafa ina nguvu ya kuingiza klabu nyingine kutoka nchi mwenyeji au kutoka ukanda mwingine wa Cecafa. Watakaocheza ni Azam na Yanga, lakini tunategemea kupokea taarifa ya Cecafa kujua ni timu gani zimetumiwa mialiko. Cecafa yenyewe itathibitisha kuwa ni nani wa ziada wamemualika, lakini wanaoingia moja kwa moja kwa Tanzania kwa vigezo ni Azam (bingwa) na Yanga wanaofaidika na uenyeji wa Tanzania”.
Kauli hii inakinzana na kauli ya Mwesigwa aliyosema na kukaririwa na mtandao huu aprili 29 mwaka huu akisema Simba wamechaguliwa kuwakilisha Tanzania.
“Mbeya City walistahili, lakini niseme ukweli, tumeamua kumchukua Simba, kwanini? kwasababu ya rekodi yake. Amekuwa bingwa mara nyingi wa mashindano haya, kwahiyo ana nafasi yake sio katika Tanzania tu bali ukanda mzima,  na huwezi kumuondoa”. Alisema Mwesigwa na kuongeza: “Mwaka jana baada ya Azam kujitoa kushiriki mashindano mapya ya kagame, tuliwapa Mbeya City nafasi”.

Hata hivyo, Mbeya City fc wanaonekana kuisubiria kwa hamu nafasi hiyo na jana kocha mkuu wa Mbeya City Juma Mwambusi alisema bado hawana uhakika wa kushiriki kutokana na kushika nafasi ya tatu 2013/2014, lakini wanatamani kuona haki inatendeka.
Wadau wa soka wanasema tayari TFF wameshatuma jina la Simba, labda kwasasa wanawatupia mzigo Cecafa ili waonekane ndio wamewachagua Simba.
Hii inatokana na ukweli kwamba wapenda soka walichukizwa na kitendo cha TFF kuwatosa Mbeya City  fc wenye sifa na kuwapa nafasi Simba wasiokuwa na vigezo na sababu kubwa ikionekana ni maslahi kuliko kuendeleza soka.


 Kwa hisani ya http://shaffihdauda.co.tz/

No comments:

Post a Comment