Wednesday, December 18, 2013
12 MAHAKAMANI KWA UKEKETAJI SAME
Wanawake 12 ambao ni
wazazi wa wasichana 21 waliofanyiwa ukeketaji wilayani Same, mkoa wa
Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi, Same, wakati waliposomewa mashitaka yao kwa mara ya kwanza tangu
wakamatwe mwishoni mwa wiki iliyopita.
Watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa kosa la
Ukatili dhidi ya watoto na kuwasababisha maumivu makali, shitaka ambalo wote
wamekana.
Tisa kati ya watuhumiwa hao 12 wameachiliwa
kwa dhamana, huku watatu wakibaki mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya
dhamana ambayo ni shilingi milioni mbili za Tanzania, sawa na dola 1250 za
Kimarekani.
Miongoni mwa washitakiwa, mmoja alikabiliwa na
mashitaka mawili, moja akiwa mzazi wa mmoja wa wasichana waliokeketwa na pia
akiwa ngariba.
Kutokana na mila na desturi ya baadhi ya
makabila nchini Tanzania, ukeketaji unafanyika japo ni kinyume cha sheria, huku
watu wanaokamatwa kuhusika na ukeketaji wakichukuliwa hatua za kisheria.
Kama watapatikana na hatia, wanawake hao
wanakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka mitano jela au kutozwa faini kubwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 30 Desemba
2013, wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Habari kwa hisani ya BBC Swahili
Waliokufa Sudan Kusini ni '400 - 500'
Mamia ya watu
wanaaminika kufa wakati wa mapigano baina ya majeshi ya yanayomuunga mkono rais
wa Sudan Kusini na yale yanayomuunga mkono makamu wa rais, maafisa wa Umoja wa
Mataifa waliopo Sudan Kusini wamesema baada ya kunukuu ripoti ambayo bado
haijathibitishwa..
Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamesema
wameambiwa na vyanzo vya habari katika mji wa Juba kwamba idadi ya watu
waliokufa wanaweza kufikia 400 hadi 500.
Sudan Kusini imekuwa na mapigano ya siku mbili
kufuatia taarifa kwamba kulikuwa na jaribio la kumpindua rais Salva Kiir.
Mwanasiasa wa upinzani aliyeko uhamishoni Riek
Machar amekana madai ya serikali kuwa alijaribu kufanya jaribio hilo.
"Kilichotokea Juba ni kutokuelewana na
mgawanyiko baina ya vikosi vya ulinzi vya rais, sio jaribio la mapinduzi,"
aliiambia Sudan Tribuni, tovuti yenye makao yake Paris katika mahojiano
yaliyochapishwa siku ya jumatano.
Bwana Machar Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan
Kusini ambaye aliondolewa na rais Kiir mwezi Julai, amesema hana taarifa wala
hausiki kwa namna yoyote na jaribio hilo la mapinduzi.
Rais wa Sudan Kusin Salva Kiir amesema kundi
la wanajeshi wanaomuunga mkono makamu wa rais Machar walikuwa wakijaribu
kujitwalia madaraka kwa kwa nguvu siku ya Jumapilil usiku, lakini walishindwa.
Wakati mapigano yanaendelea siku ya jumatatu
na jumanne, serikali imesema wanasiasa kumi maarufu akiwemo waziri wa zamani wa
fedha, wametiwa mbaroni.
Taarifa za mapigano hayo zimefika kwenye
baraza la kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya jumanne, ambapo limesema
mapigano hayo yanaweza kuwa mapingano ya kikabila.
Tuesday, December 17, 2013
Subscribe to:
Posts (Atom)