Wednesday, December 18, 2013

Waliokufa Sudan Kusini ni '400 - 500'


Mamia ya watu wanaaminika kufa wakati wa mapigano baina ya majeshi ya yanayomuunga mkono rais wa Sudan Kusini na yale yanayomuunga mkono makamu wa rais, maafisa wa Umoja wa Mataifa waliopo Sudan Kusini wamesema baada ya kunukuu ripoti ambayo bado haijathibitishwa..
Wanadiplomasia wa Umoja wa Mataifa wamesema wameambiwa na vyanzo vya habari katika mji wa Juba kwamba idadi ya watu waliokufa wanaweza kufikia 400 hadi 500.
Sudan Kusini imekuwa na mapigano ya siku mbili kufuatia taarifa kwamba kulikuwa na jaribio la kumpindua rais Salva Kiir.
Mwanasiasa wa upinzani aliyeko uhamishoni Riek Machar amekana madai ya serikali kuwa alijaribu kufanya jaribio hilo.
"Kilichotokea Juba ni kutokuelewana na mgawanyiko baina ya vikosi vya ulinzi vya rais, sio jaribio la mapinduzi," aliiambia Sudan Tribuni, tovuti yenye makao yake Paris katika mahojiano yaliyochapishwa siku ya jumatano.
Bwana Machar Makamu wa Rais wa zamani wa Sudan Kusini ambaye aliondolewa na rais Kiir mwezi Julai, amesema hana taarifa wala hausiki kwa namna yoyote na jaribio hilo la mapinduzi.
Rais wa Sudan Kusin Salva Kiir amesema kundi la wanajeshi wanaomuunga mkono makamu wa rais Machar walikuwa wakijaribu kujitwalia madaraka kwa kwa nguvu siku ya Jumapilil usiku, lakini walishindwa.
Wakati mapigano yanaendelea siku ya jumatatu na jumanne, serikali imesema wanasiasa kumi maarufu akiwemo waziri wa zamani wa fedha, wametiwa mbaroni.
Taarifa za mapigano hayo zimefika kwenye baraza la kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya jumanne, ambapo limesema mapigano hayo yanaweza kuwa mapingano ya kikabila.


No comments:

Post a Comment