Wanawake 12 ambao ni
wazazi wa wasichana 21 waliofanyiwa ukeketaji wilayani Same, mkoa wa
Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi, Same, wakati waliposomewa mashitaka yao kwa mara ya kwanza tangu
wakamatwe mwishoni mwa wiki iliyopita.
Watuhumiwa wote wanashitakiwa kwa kosa la
Ukatili dhidi ya watoto na kuwasababisha maumivu makali, shitaka ambalo wote
wamekana.
Tisa kati ya watuhumiwa hao 12 wameachiliwa
kwa dhamana, huku watatu wakibaki mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya
dhamana ambayo ni shilingi milioni mbili za Tanzania, sawa na dola 1250 za
Kimarekani.
Miongoni mwa washitakiwa, mmoja alikabiliwa na
mashitaka mawili, moja akiwa mzazi wa mmoja wa wasichana waliokeketwa na pia
akiwa ngariba.
Kutokana na mila na desturi ya baadhi ya
makabila nchini Tanzania, ukeketaji unafanyika japo ni kinyume cha sheria, huku
watu wanaokamatwa kuhusika na ukeketaji wakichukuliwa hatua za kisheria.
Kama watapatikana na hatia, wanawake hao
wanakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka mitano jela au kutozwa faini kubwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 30 Desemba
2013, wakati uchunguzi zaidi ukiendelea.
Habari kwa hisani ya BBC Swahili
No comments:
Post a Comment