Thursday, June 6, 2013

Vigogo wanne upinzani wafikishwa mahakamani vurugu za Mtwara

Viongozi wanne wa vyama vya upinzani mkoani Mtwara, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara, wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo kula njama, kufanya uchochezi na kuamsha hisia mbaya kwa wakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Washtakiwa hao ni Katani Ahmed Katani (33) na Saidi Kulaga (45) wa CUF, Hassan Uledi (35) wa NCCR Mageuzi, Hamza Licheta (51) wa TLP, wote wakazi wa Mtwara.
Awali Katani, Uledi na Licheta walifikishwa mahakamani Mei 31 mbele ya Hakimu Mfawidhi Mwandamizi, Dainess Lyimo, kabla ya kuunganishwa na Kulaga ambaye alikamatwa Juni 2 mwaka huu na kufikishwa mahakamani peke yake Juni 3.
Hata hivyo, juzi washtakiwa wote wanne waliunganishwa na kufikishwa kwa Hakimu Mkazi Mussa Esanju, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa Hakimu Lyimo yupo safarini.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Justine Sanga, alidai washtakiwa hao kwa pamoja walikutana mahali na muda usiojulikana na kula njama hizo.
Sanga alidai shtaka la pili, Januari 16, mwaka huu eneo la Bima mjini Mtwara, washtakiwa kwa pamoja walidaiwa kufanya makosa ya uchochezi, kwa kutoa hotuba kwa wakazi hao, kwa lengo la kuleta chuki na kusababisha kuharibu mali za umma na binafsi.
Pia, alidai shtaka la tatu Januari 16, mwaka huu eneo la Bima washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuamsha hisia mbaya, kufanya mikutano ya kisiasa, kutoa maneno makali na kusababisha kuamsha hisia mbaya za wananchi.
Wakili wa utetezi, Banana Biboze aliomba mahakama kumwachia mteja wake, Hassan Uledi, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (Mum) kwa ajili ya maandalizi ya mitihani yake Juni 16, mwaka huu.
Hata hivyo, mahakama haitoa dhamana kwa washtakiwa hao kwa kile kilichodaiwa ni kwa ajili ya usalama wa washtakiwa na jamii na kwamba, Hakimu Lyimo anayesikiliza kesi hiyo yupo safarini.
Washtakiwa kwa pamoja walikana mashtaka na kurudishwa rumande hadi Juni 13, mwaka huu.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment