MTIKISIKO mkubwa wa kisiasa jana
umelikumba taifa, baada ya wafuasi wa Chadema kupambana na polisi katika maeneo
mbalimbali.
Hali hiyo,
ilianza kuonekana mapema jijini Dar es Salaam, wakati Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe aliwapowasili Makao Makuu ya Jeshi la Polisi saa tano asubuhi kwa
ajili ya kuhojiwa.
Mbowe
aliitwa kuhojiwa na viongozi wa jeshi hilo kwa madai ya kutoa kauli za
uchochezi wiki iliyopita.
Akizungumza kwenye mkutano wa
Kamati Kuu ya chama chake, Mbowe alisema wataitisha maandamano na migomo
isiyokuwa na kikomo nchi nzima kuishinikiza Serikali kusitisha Bunge Maalumu la
Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
Mbowe
aliwasili polisi saa 5 asubuhi akisindikizwa na msafara wa magari matano
yaliyobeba baadhi ya wanachama, mawakili na viongozi wa chama hicho.
Baada ya
kuwasili katika eneo hilo, wanachama hao walipinga kiongozi wao kushuka ndani
ya gari hadi atakapoingia ndani ya lango kuu.
Wanachama
hao walisikika wakisema ‘Peoples’ huku wengine wakiitikia ‘Power’.
Kitendo
hicho kilipingwa na polisi waliokuwa wakilinda lango hilo na kuamuru Mbowe
ashuke na kuingia kwa miguu ndani ya jengo hilo.
Kitendo
hicho kilionekana kuwakera wafuasi waliokuwa wamekusanyika eneo hilo na kuamua
kusukuma lango hilo kwa nguvu ili waweze kuingia pamoja na kiongozi wao.
Kutokana
na hali hiyo, wafuasi hao waligoma na kuanza kupambana na polisi ambao nao
walijihami kwa kuzuia geti la lango wakiwa ndani.
Baada ya
mabishano ya muda mrefu, ndipo polisi walipokubali Mbowe aingie na gari ndani
ya jengo hilo huku wakizuia msafara wa magari mengine.
Kutokana
na uamuzi huo, mawakili walilazimika kushuka ndani ya gari.
Mmoja wa
askari aliyekuwa getini hapo, alisikika akisema anayepaswa kuingia ndani ya
jengo ni Mbowe na mawakili wake.
“Tumekubaliana
gari linaloingia ndani ni moja tu la mwenyekiti, msilazimishe matumizi ya
nguvu,” alisikika akisema askari huyo.
Kitendo
hicho kilipingwa na wanachama hao huku wakitaka wabunge, mawakili na viongozi
wengine waingie ndani.
Kutokana
na hali hiyo, polisi walikubali na kuwaruhusu viongozi hao kuingia ndani huku
wakiwaamuru wanachama wengine na waandishi wa habari kusimama umbali wa mita
200 kutoka kwenye lango hilo.
Baada ya
kutokea kwa tangazo hilo, wafuasi hao walikaidi amri hiyo na kusababisha askari
D. D. Zahoro kuamuru kutumika nguvu kuwatawanya pamoja na waandishi wa habari
hali iliyosababisha kujitokeza kwa vurugu katika eneo hilo.
Vurugu
hizo zilidumu kwa muda wa saa moja na kusimamisha shughuli mbalimbali
zinazoendelea ndani ya jengo hilo na njia kufungwa kwa muda.
Katika
vurugu hizo,wafuasi wanne wa chama hicho walikamatwa.
MWANDISHI
APIGWA
Katika
tukio hilo, mwandishi wa habari wa Gazeti la Tanzania Daima, Josephat Isango
alijikuta akishambuliwa vibaya na askari kwa virungu.
Licha ya
Isango kuonyesha kitambulisho, polisi hawakutaka kumsikiliza zaidi ya kuendelea
kumshushia kipigo na kumsababishia maumivu katika mguu wa kulia.
Kipigo
hicho kilisitishwa baada ya waandishi wengine kupiga kelele kuwaomba polisi
kumwachia kwa sababu alikuwa kwenye majukumu yake ya kazi.
MBOWE
AHOJIWA
Wakati
tukio hilo likiendelea, Mbowe alikuwa ndani ya jengo hilo akiendelea
kuhojiwa akiwa na mawakili wake sita.
Mawakili
hao, ni Peter Kibatala, Profesa Abdallah Safari, Mabere Marando, Nickson
Tugala, Tundu Lissu na John Malya.
Mahojiano
hayo yalianza saa tano na kudumu kwa zaidi ya saa nne. Ilipofika saa 8:49
mchana, mawakili wanne wakiongozwa na Lissu walitoka nje na kuzungumza na
wafuasi na waandishi wa habari.
“Mwenyekiti
yuko salama, aliitwa kwa ajili ya mahojiano na yamefanyika vizuri chini ya
mawakili.
“Polisi
wameomba tuzungumze na nyie tuwaombe muondoke kwa sababu mwenyekiti akitoka na
mkiwa wengi kunaweza kukawa na uvunjifu wa amani,” alisema Lissu.
Baadhi ya
wanachama hao walisikika wakisema hawawezi kuondoka kwa sababu hawawaamini
polisi.
“Sisemi
nawaamini polisi au la, tumekubaliana kwamba mwenyekiti atapata dhamana, hivyo
haitakuwa busara tukiondoka kwa maandamano, tulikuja kwa amani hatutaki mtu
atoke hapa akiwa amedhurika,” alisema Lissu.
Baadhi ya
wafuasi walikubali kuondoka huku wengine wakibaki.
Saa 9:17
alasiri, Mbowe alitolewa kwa kupitia mlango wa nyuma wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, huku akisindikizwa na magari manne kwenda Kituo cha Polisi Kati
ambako aliachiwa kwa dhamana.
MTIKILA
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha DP, Mchungaji Christopher
Mtikila alifika eneo hilo akiwa kwenye bajaj, lakini alizuiwa kuingia ndani.
DODOMA
Polisi
mjini Dodoma, jana waliimarisha ulinzi kwa ajili ya kupambana na wafuasi wa
Chadema waliopanga kuandamana kupinga Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea
mjini humo.
Miongoni
mwa maeneo yaliyokuwa na ulinzi mkali ni pamoja na jengo la Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Viwanja vya Nyerere Square na mitaa mbalimbali ya mjini
hapo.
Polisi
waliweka uzio wa kamba kilipo Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na makutano ya
barabara jirani na stendi ya mabasi ya abiria yanayokwenda mikoani ili
kutoruhusu watu na magari kuelekea eneo la Bunge.
Jengo la
Bunge lilikuwa limezungukwa na askari wengi wenye silaha, farasi na mbwa
kuhakikisha usalama unakuwapo katika eneo hilo.
Ndani ya
eneo la Bunge, nako ulinzi ulikuwa mkali kwani kulikuwa na idadi kubwa ya
askari waliokuwa na silaha pamoja na mbwa.
Viwanja
vya Nyerere
Katika
viwanja vya Nyerere ambako wakazi wa Dodoma hupenda kukusanyika kwa ajili ya
kupumzika na kupata huduma za chakula na vinywaji, jana shughuli zilisimama kwa
muda kwa kuwa polisi walikuwa wameweka ulinzi tangu asubuhi.
Nje ya
viwanja hivyo, kulikuwa na vijana waliokuwa na mabango likiwamo lililosomeka
‘Sitta tumia busara ahirisha Bunge la Katiba’.
Katika
viwanja hivyo, polisi walionekana wakiwa wamekamata vijana wapatao kumi
waliodaiwa kuwa walikuwa wakitaka kuandamana.
Wakati
hali ikiwa hivyo katika maeneo hayo, ulinzi pia uliimarishwa katika mitaa
mbalimbali ya mji huo kwani askari polisi waliokuwa na silaha na askari kanzu,
walikuwa wametanda kila kona.
Chini ya
ulinzi huo, magari yaliyokuwa yamejaa askari polisi yakiwamo ya askari wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), yalikuwa yakizunguka kila kona kuhakikisha
hakuna maandamano yatakayofanyika.
Gari la
Chadema
Pamoja na
askari kuimarisha ulinzi huo, gari la Chadema lenye namba za usajili T 792 CAX
likiwa na nembo ya M4C, nalo lilikuwa likipita katika mitaa ya mji huo ingawa
haikufahamika lilikuwa likifanya hivyo kwa maana gani.
Kuanzia
saa 12 alfajiri jana, ofisi za Chadema Mkoa wa Dodoma zilizoko eneo la Mji
Mpya, zilikuwa zikilindwa na askari polisi waliokuwa na silaha.
Radio za
kijamii zafungwa
Katika
hali ambayo haikujulikana wazi, radio za kijamii za mjini hapa hazikuwa hewani
jana asubuhi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kudhibiti mawasiliano kati ya
Chadema na wananchi.
Taarifa
zilizopatikana baada ya mawasiliano hayo kukatika, zinasema redio hizo hazikuwa
hewani kwa saa kadhaa jana kwa vile viongozi wa Chadema walikuwa wakizitumia
kuhamasisha wananchi.
Miongoni
mwa waliodaiwa kutumia redio hizo ni Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma,
Jella Mambo ambaye awali alihamasisha maandamano hayo kupitia Redio Kifimbo na
Nyemo FM.
Hata
hivyo, taarifa nyingine zinasema redio hizo hazikuwa hewani kwa kuwa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) walikuwa wakifanya marekebisho ya masafa.
Akizungumza
na MTANZANIA jana, Mambo alikiri kutumia redio hizo kuhamasisha maandamano kwa
kuwa yalikuwa halali.
Pamoja na
hayo, alisema kama Jeshi la Polisi limedhamiria kudhibiti maandamano yao,
linatakiwa kuandaa fedha nyingi ili kukabiliana nayo.
“Hapa
Dodoma maandamano yapo ila tunayafanya kimkakati kwani watu wametawanyika
maeneo mbalimbali kila mmoja ana mabango yenye ujumbe tofauti, yakiwamo
tunayompongeza Rais Jakaya Kikwete kwa busara yake aliyoitumia kutaka mchakato
wa Katiba Mpya usikamilike kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” alisema
Mambo.
Wakati huo
huo, Mambo alisema gari moja la Chadema lililokuwa limebeba wajumbe wa Mkutano
Mkuu waliokuwa wakitoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza, lilikamatwa na askari
polisi.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Emannuel Lukura alikiri kukamatwa kwa gari na
wafuasi wanne wa chama hicho.
MBEYA
Habari
kutoka mkoani Mbeya, zinasema polisi wameendelea kutunushiana misuli na Chadema
kuhusu kufanyika au kutofanyika kwa maandamano ya kupinga kuendelea kwa Bunge
Maalumu la Katiba.
Chadema
imesisitiza kufanyika kwa maandamano hayo leo. Mratibu Kanda za Nyanda za Juu
Kusini, Franky Mwaisumbe aliliambia MTANZANIA jana kuwa licha ya polisi kudai
kuwa maandamano hayo ni batili, wao watahakikisha yanafanyika kwani lengo lao
ni kufikisha ujumbe kwa wananchi.
Alisema
wao wanachokifanya ni kutimiza azimio la Kamati Kuu lililotolewa wiki iliyopita
na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema hadi jana jioni maandamano hayo
yalikuwa hayajaombewa kibali.
ARUSHA
Mkoani
Arusha, Chadema kimethibitisha kufanya maandamano leo, huku kikisema tayari
majimbo 14 kati ya 33 yamewasilisha barua katika vituo vya polisi kwa ajili ya
taarifa.
Katibu wa
Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu
jana, alisema tayari wamekwishajipanga kuhakikisha wanafanya maandamano ya
amani ambayo hayatasababisha usufumbufu kwa watu wala kuvunja sheria yoyote.
“Lengo
letu ni ujumbe ufike kwa wabunge Dodoma, kwamba kikao wanachoendelea nacho
hakitatupa Katiba mpya. Sasa maandamano haya tumeyapa kwa mfumo wa pekee
kabisa,” alisema.
Habari hii
kwa hisani ya Gazeti la Mtanzania