Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema hakuna
uwezekano wa kubadili muundo wa muungano kutoka Serikali mbili kwenda Serikali
tatu katika mchakato wa Katiba.
Kauli ya Balozi Sefue imekuja ikiwa ni siku chache tangu Rais
Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa Kituo cha Demokrasia (TCD) na kutoa
uamuzi wa kuahirisha mchakato wa Katiba hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2015.
Suala la muundo wa muungano lilichukua mjadala mkali ndani ya
Bunge Maalumu la Katiba huku wajumbe wanaounda kundi la Ukawa wakiunga mkono
mapendekezo ya Rasimu ya Katiba ya muundo wa Serikali tatu na wajumbe wa CCM
wakisisitiza muundo wa Serikali mbili.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Balozi
Sefue alisema mchakato wa Katiba unahitaji maridhiano, lakini suala la muundo
wa muungano halina maridhiano katika jamii hivyo litachelewesha upatikanaji wa
Katiba:
“Katika historia ya nchi yoyote, wakati unafika wananchi wakawa
na maridhiano fulani, wakaamua kuyaingiza ndani ya Katiba. Tatizo linajitokeza
pale watu au makundi fulani yanapong’ang’ania kuingiza ndani ya Katiba mambo
ambayo ni dhahiri hayana maridhiano ndani ya jamii. Mfano ni suala la muundo wa
Muungano,” alisema na kuongeza:
“Uzoefu wa Bunge Maalumu hadi sasa ni kuwa hakuna uwezekano wa
kupata maridhiano ya kubadili muundo wa Muungano kutoka Serikali mbili kwenda
tatu. Hutapata maridhiano hayo ndani ya Bunge Maalumu na hutapata maridhiano
ukienda kwa wananchi,” alisema.
Alisema anaamini wajumbe wa Bunge Maalumu walifanya uamuzi wa
busara kuliweka kando jambo hilo linalotugawa, na kuendelea kujadili Rasimu ya
Katiba kwa msingi wa mfumo uliopo wa Serikali mbili,” alisema.
Balozi Sefue aliongeza kuwa tangu suala hilo liwekwe kando
kumekuwa na kasi na matumaini ya kupata Katiba Mpya.
Alisema jambo hilo ni kubwa na uzoefu unaonyesha lina uwezo
mkubwa wa kutugawa na kuchelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Balozi Sefue alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliamini
yatapatikana maridhiano kuhusu kubadili muundo wa Muungano, ilivyo sasa, ni
wazi kuwa maridhiano kuhusu mabadiliko hayo hayapo na hayatapatikana.
“Hakuna idadi ya makongamano na maandamano yatakayobadili hali
hiyo sasa,” alisema.
Licha ya kusema kuwa kuna matumaini ya kupata Katiba Mpya,
Balozi Sefue alisema ikishindikana Katiba iliyopo itafanyiwa marekebisho ili
ituvushe hadi mchakato utakaporejeshwa tena.
Kwa hisani ya http://www.mwananchi.co.tz/
No comments:
Post a Comment