Rais Jakaya Kikwete amewaonya
viongozi wanaoleta mvutano juu ya wapi ipitishwe Barabara ya
Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo kwa kuwa wanaendesha ubishani
unaoweza kuwachanganya wataalamu walioshughulikia suala hilo.
Amesema baada ya kumalizika kwa barabara ya
Tanga-Horohoro,Serikali yake sasa kwa Mkoa wa Tanga itaelekeza nguvu
zake katika ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo.
Alisema hayo juzi alipokuwa akifungua barabara
mpya ya kiwango cha lami ya Tanga-Horohoro katika sherehe zilizofanyika
kwenye kituo kipya cha mabasi cha Wilaya ya Mkinga kilichopo Kasera
wilayani hapa.
Barabara hiyo ya Tanga- Horohoro ya urefu wa
kilometa 65 imejengwa na Kampuni ya kutoka China ya Sinohydro
Corporation Ltd iliyokabidhiwa rasmi kazi hiyo Januari 4, mwaka 2010
baada ya kuingia mkataba baina yake na mfadhili ambaye ni mfuko wa
Millenium Challenge (MCC) na Serikali ya Tanzania kwa gharama ya Sh69.8
bilioni. Akizungumza katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na mabalozi wa
kutoka nchi za Marekani, India, Kenya, watendaji wakuu wa MCC, mawaziri,
wakuu wa mikoa ya Tanga, Pwani na wananchi, Rais Kikwete aliwaonya
wanaoleta mvutano juu ya barabara hiyo kwamba wanawavuruga wataalamu.
Alikuwa akizungumzia juu ya mvutano uliojitokeza
kuhusu wapi ipite barabara hiyo, ambapo wapo wanaokubaliana na wataalamu
wanaotaka ipitie ndani ya Hifadhi ya Mbuga ya Taifa ya Saadani huku
wengine wakiwamo wanamazingira wakipinga kwa madai kwamba ikipitishwa
katikati itawafukuza wanyama waliomo.
Hotuba hiyo ya Rais Kikwete ni majibu kwa kamati
ya ushauri mkoa wa Tanga ambayo katika kikao chake kilichofanyika mwezi
uliopita ulijitokeza mvutano wa wapi ipitishwe barabara huku wajumbe
wengine wakitaka ipite katikati ya hifadhi na wengine wakihadharisha
kuwa itaathiri ustawi wa wanyama.
Katika kikao hicho kilichofanyika chini ya
uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, wajumbe waliagiza
iandikwe barua kwa Rais Jakaya Kikwete kumuomba kukubali pendekezo la
kupitisha barabara nje ya hifadhi.
Barabara hiyo kama itapitishwa katika hifadhi ya
Saadani itakuwa ya urefu wa kilomita 175 na ikiwa itazungushwa na
kupitishwa nje ya hifadhi italazimika kuongezeka urefu wa kilomita 35
nyingine ambapo kwa sasa ipo kwenye hatua ya kufanyiwa usanifu.
Barabara hii ya Bagamoyo-Saadan-Pangani –Tanga
itajengwa kwa ushirikiano wa nchi za Jumiya ya Afrika Mashariki,ambapo
kwa upande wa Kenya mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara ya
Horohoro-Lungalunga-Mombasa hadi Malindi.
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment