SHIRIKISHO la soka
Tanzania, TFF, limeshindwa kuthibitisha moja kwa moja kama ni Simba au Mbeya
City fc itakayoshiriki kombe la klabu bingwa Afrika mashariki na kati, maarufu
kwa jina la ‘Kagame Cup’ linalotarajia kuanza kutimua vumbi Julai 11 hadi
Agosti 2 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Katibu mkuu wa TFF,
Mwesigwa Selestine ameuambia mtandao huu kuwa CECAFA ndio watakaosema ni timu
gani ya tatu nchini Tanzania wameialika kushiriki Kagame.
Kauli hii
inatofautiana na ile aliyowahi kusema kupitia mtandao huu kuwa TFF wameichagua
Simba badala ya washindi wa tatu wa msimu wa 2013/2014 wa ligi kuu soka
Tanzania bara, Mbeya City fc.
“Kimsingi na kwa
taratibu wawakilishi wa Tanzania ni bingwa wa msimu uliopita (2013/2014) ambao
ni Azam na mshindi wa pili ambaye ni Yanga anayefaidika na uenyeji wa
Tanzania”. Amesema Mwesigwa na kuongeza: “Lakini Cecafa ina nguvu ya kuingiza
klabu nyingine kutoka nchi mwenyeji au kutoka ukanda mwingine wa
Cecafa. Watakaocheza ni Azam na Yanga, lakini tunategemea kupokea taarifa
ya Cecafa kujua ni timu gani zimetumiwa mialiko. Cecafa yenyewe itathibitisha
kuwa ni nani wa ziada wamemualika, lakini wanaoingia moja kwa moja kwa Tanzania
kwa vigezo ni Azam (bingwa) na Yanga wanaofaidika na uenyeji wa Tanzania”.
Kauli hii inakinzana
na kauli ya Mwesigwa aliyosema na kukaririwa na mtandao huu aprili 29 mwaka huu
akisema Simba wamechaguliwa kuwakilisha Tanzania.
“Mbeya City
walistahili, lakini niseme ukweli, tumeamua kumchukua Simba, kwanini? kwasababu
ya rekodi yake. Amekuwa bingwa mara nyingi wa mashindano haya, kwahiyo ana
nafasi yake sio katika Tanzania tu bali ukanda mzima, na huwezi
kumuondoa”. Alisema Mwesigwa na kuongeza: “Mwaka jana baada ya Azam
kujitoa kushiriki mashindano mapya ya kagame, tuliwapa Mbeya City nafasi”.
Hata hivyo, Mbeya City
fc wanaonekana kuisubiria kwa hamu nafasi hiyo na jana kocha mkuu wa Mbeya City
Juma Mwambusi alisema bado hawana uhakika wa kushiriki kutokana na kushika
nafasi ya tatu 2013/2014, lakini wanatamani kuona haki inatendeka.
Wadau wa soka wanasema
tayari TFF wameshatuma jina la Simba, labda kwasasa wanawatupia mzigo Cecafa
ili waonekane ndio wamewachagua Simba.
Hii inatokana na
ukweli kwamba wapenda soka walichukizwa na kitendo cha TFF kuwatosa Mbeya City
fc wenye sifa na kuwapa nafasi Simba wasiokuwa na vigezo na sababu kubwa
ikionekana ni maslahi kuliko kuendeleza soka.
No comments:
Post a Comment