Friday, March 15, 2013

Utekaji, uuaji watu Tanzania: Nani atafuata baada ya Kibanda?

Hali ya usalama nchini inaonekana kutia shaka wananchi hasa kufuatia mfululizo wa matukio ya watu kutekwa, kuteswa hata kuuawa.
Kwa bahati mbaya ni kwamba kadri siku zinavyokwenda mbele, vitendo vya watu kutekwa vinaonekana kuongezeka, huku hofu kuu ikiwa ni nini kinachosababisha hayo au akina nani hasa walioko nyuma ya vitendo hivyo vinavyoonekana kutishia maisha watu.
Watanzania waliowahi kutekwa
Baadhi ya watu ambao wameuawa katika mazingira yenye utata ama yanayofanana nay a utekaji ni mwanasheria maarufu nchini, Profesa Jwani Mwaikusa. Msomi huyu ambaye alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitivo cha sheria, aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa nje ya nyumba yake, huku wauaji wakiondoka bila kupora chochote zaidi ya mkoba na makaratasi aliyokuwa nayo.
Profesa anakumbwa kwa mengi, mojawapo ni kwamba alikuwa mmoja wa mawakili walikuwa wakiwatetea washtakiwa wa mauaji ya kimbali  Rwanda. Alikuwa akimtetea mfanyabiashara maarufu nchini Rwanda, Yussuf Munyakazi aliyekuwa akihusishwa na mauaji hayo katika kesi iliyokuwa ikiendelea katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), jijini Arusha.
Aliyekuwa akimtetea afungwa
Hata hivyo ICTR ilimtia hatiani Munyakazi kwa kumfunga miaka 25 kwa maelezo kuwa alihusika kwa namna moja ama nyingine kuendesha mauaji ya kimbari na kuteketeza familia huko Rwanda.

Munyakazi katika mashtaka yake alitakiwa na Serikali ya Rwanda akashtakiwe nchini kwao, lakini alikataa kwa kuhofia kutotendewa haki.Ni jitihada za Profesa Mwaikusa, zilizosababisha kesi yake iendeshwe ICTR Arusha hadi ilipotolewa hukumu.
Wakati hukumu inatolewa, Profesa Mwaikusa alishauawa na watu wasiojulikana, jijini Dar es Salaam, kitendo ambacho kinaonekana kumuumiza Munyakazi, kutokana na ukweli kuwa msomi huyo alikuwa ana uwezo mkubwa katika masuala ya sheria, kiasi cha kufanikisha asipelekwe Rwanda, kama Serikali ya nchi hiyo ilivyotaka.
Mhadhiri huyo  mahiri aliuawa nyumbani kwake barabara ya Makonde eneo la Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Wakati Mwaikusa akijiandaa kushuka katika gari lake, watu hao walimgongea kioo na kumwamuru kushuka, inaelezwa kuwa Profesa Mwaikusa alisita, ndipo walimpommiminia risasi hadi kufa.
Wakati wamemaliza kumpiga risasi, alitokea mpwae Profesa Mwaikusa, Gwamaka Daudi (25), kwa lengo la kumnusuru, kwa bahati mbaya naye aliuawa kwa kupigwa risasi mgongoni.
Baada ya kuwaua ndugu wawili, watu hao walianza kutoweka, kwa mbele wakaona kikundi cha watu ambalo walilitilia shaka kwamba wanataka kupambana nao, ndipo walipompiga risasi mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la John Mtui (45).
Kama hiyo haitoshi matukio mengine zaidi ya watu kutekwa na hata kuuawa yanaonekana kuendelea.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment