Tuesday, May 21, 2013

John Kerry kuzuru mashariki ya kati na Afrika



Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry anatarajiwa kusafiri kwenda katika mataifa ya mashariki ya kati na Afrika kuanzia Jumanne ijayo kwa ziara itakayomchukua hadi Mei 27.
Kerry  anatarajiwa  kuanza ziara  yake  mjini  Muscat  siku ya  Jumanne (21.05.2013), ikifuatiwa  na  Jordan  siku  ya  Jumatano, ambako atakutana  na  kile  kinachoitwa  "washirika  muhimu  wa  kimataifa", kuangalia uwezekano  wa  kupatikana  kwa  suluhisho  la  kisiasa kupitia  majadiliano  nchini  Syria , wizara  ya  mambo  ya  kigeni nchini  Marekani  imesema  katika  taarifa.
Mkutano  huo  unakuja  kabla  ya  mkutano  mkubwa  wa  kimataifa kuhusu  Syria unaopangwa  na  Urusi  na  Marekani , na  ambao unatarajiwa  kufanyika  mwezi  ujao.
Kerry akiwa katika majadiliano na rais Putin wa Urusi
Siku  ya  Alhamis  na  Ijumaa , Kerry anatarajiwa  kuzuru  Jerusalem na  Ramallah  kufuatilia  mazungumzo  juu  ya  kuleta  pamoja  Israel na  Palestina  katika  meza  ya  majadiliano, kujadili amani, taarifa hiyo  imesema.


Pia  siku  ya  Ijumaa , Kerry  anatarajiwa  kusafiri  kwenda  mjini Addis Ababa kushiriki  katika  sherehe  za  siku  mbili  za kuadhimisha  miaka  50  tangu  kuundwa  kwa  Umoja  wa  nchi  za Afrika  OAU, ambao  hivi  sasa   unajulikana  kama  Umoja  wa Afrika, AU. viongozi  kutoka  sehemu  mbali  mbali  za  Afrika watahudhuria  sherehe  hizo.
Hapo  Mei 26 , waziri  Kerry  anapanga  kurejea  mjini  Amman Jordan  kushiriki  katika  jukwaa  la  kiuchumi  la    dunia.
Wakati  huo huo  baraza  la  usalama  la  umoja  wa  mataifa  linatafakari ombi kutoka  kwa  maafisa  wa  ngazi  ya  juu  wa  shirika  la  misaada  la umoja  huo  linalodai  kufikishwa  kwa  misaada  katika  nchi iliyoharibiwa  kwa  vita  ya  syria, hatua  ambayo  inaweza kusababisha  hali  ya  mivutano  baina  ya  Urusi  na  mataifa  ya magharibi  kuhusiana  na  upelekaji  wa  misaada  ya  kiutu  kupitia mipakani, wamesema  wanadiplomasia  wa  Umoja  wa  Mataifa.

No comments:

Post a Comment