Friday, May 3, 2013

260,000 WALIKUFA KWA UKAME SOMALIA

Watoto wengi walikufa kwa Utapia mlo
Takriban watu 260,000 walifariki dunia wakati wa ukame ulioikumba Somalia kuanzia mwaka 2010 hadi 2012, utafiti umebaini.
Nusu ya waliofariki dunia walikuwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano, inaeleza ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, pamoja Mtandao wa Kuonya Mapema Kuhusu Majanga ya Ukame unaofadhiliwa na Marekani.
Idadi ya vifo ilikuwa kubwa kuliko ile iliyokadiriwa ya watu 220,000 waliofariki wakati wa ukame wa mwaka 1992.
Janga hilo lilisababishwa na ukame mkali, uliochochewa na mapigano kati ya makundi hasimu yaliyokuwa yakigombea madaraka.
Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ulitangaza hali ya ukame Julai 2011 katika mikoa ya Somalia ya Bakool uliopo kusini na ule wa chini wa Shabelle, ambayo ilikuwa inadhibitiwa na kundi la wanamgambo wa Al – Shabab wenye mafungamano na Al – Qaeda.
Lakini kundi hilo lilikanusha kuwepo kwa hali hiyo na kuyapiga marufuku mashirika kadhaa ya misaada ya nchi za magharibi kufanya shughuli zake katika maeneo hayo.
Baadaye ukame ulisambaa katika maeneo mengine ukiwemo mkoa wa kati wa Shabelle na Afgoye na katika kambi za watu wasiokuwa na makaazi katika maeneo yaliyokuwa yakidibitiwa na serikali katika mji mkuu Mogadishu.
Mchumi Mwandamizi wa shirika la FAO, Mark Smulders amesema, ukweli kuhusu ukubwa wa janga hilo la kibinadamu umeibuka kwenye utafiti uliofanywa kwa kushirikiana na Mtandao wa Kuonya Mapema Majanga ya Ukame, Fews Net.
“Kwa kawaida, kukadiria vifo wakati wa dharura ni sayansi isiyo rasmi, lakini kutokana na ubora na kiwango cha takwimu zilizokuwepo, tuna uhakika na utafiti huo”, amesema ofisa wa Fews Net Chris Hillbruner.
“Utafiti huo unaeleza kuwa, kilichotokea Somalia ni moja ya majanga mabaya kabisa ya ukame kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, “ ameongeza.
Inakadiriwa kuwa 4.6% ya jumla ya idadi ya watu na 10% ya watoto chini ya umri wa miaka mitano walifariki dunia huko maeneo ya kusini na kati mwa Somalia, imeeleza ripoti hiyo.
“Ripoti hiyo imethibitisha kuwa hatua za ziada zingechukuliwa kabla ya ukame huo haujatangazwa, amesema Phillippe Lazzarini, Mratibu wa Shughuli za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.
Somalia ilikumbwa na ukame mkali mwaka 2011, ulioathiri zaidi ya watu milioni 13 katika eneo lote la Pembe ya Afrika.
Maelfu ya watu walikimbia makaazi yao wakisaka chakula. Umoja wa mataifa ulitangaza ukame huo kumalizika Februari 2012.
Kwa zaidi ya miaka 20 ya vita vya weyewe kwa wenyewe, Somalia imeshuhudia wababe wa kivita wa koo, wanasiasa mahasimu na vikundi vya wanamgambo vikigombea madaraka, hali iliyoruhusu kushamiri kwa ukosefu wa utawala wa sheria.
Septemba mwaka jana, serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa iliingia madarakani baada ya miaka nane ya utawala wa mpito, hatua iliyoleta utengamano katika baadhi ya maeneo.

No comments:

Post a Comment