Monday, May 20, 2013

Chuji atwaa tuzo ya SuperSport ya mchezaji bora wa mechi


Dar es Salaam. Kiungo wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ ametwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi ya kituo cha SuperSport katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya Simba iliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Chuji alionyesha kiwango cha juu katika mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki 57,406 kwa kuiunganisha vyema safu ya kiungo ya Yanga.
Baada ya mechi hiyo kituo cha SuperSport kilichoonyesha mechi hiyo moja kwa moja kilimtangaza Chuji kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kuwafunika Didier Kavumbagu na Hamisi Kiiza wafungaji wa mabao ya Yanga.
Chuji alisema tuzo hiyo ameipokea kama changamoto kubwa kwake katika kuhakikisha anaendelea kucheza kwa kiwango cha juu siku zote.
“Nimefurahi kusikia hivyo sababu SuperSport ni watu wa mpira na watakuwa wameona uwezo wangu katika mechi hii, lakini hali hiyo naichukua kama moja ya changamoto kwangu,” alisema Chuji. Yaliyostaajabisha kipute cha watani wa jadi kama kawaida ya mtanange wa watani wa jadi yaani  Simba na Yanga huwa haukosi  matukio mageni ambayo huacha simulizi kwa mashabiki.
Haya ni baadhi tu matukio yaliyojiri kwenye mchezo huo uliopigwa mwishoni mwa wiki kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mwamuzi aanguka, mpira wasimama
Mashabiki wa soka walipigwa na “bumbuwazi” baada ya mwamuzi Martin Saanya aliyekuwa anachezesha mpambano huu wa Simba na Yanga kulala chini ghafla.
Tukio hili ambalo ni nadra kutokea kwenye viwanja  vya soka lilisababisha mpira kusimama kwa muda mrefu, ingawa ilikuja kubainika kwamba alipigwa kiwiko wakati akisuluhisha ugomvi baina na beki Said Nasoro ‘Cholo’ wa Simba na mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu.

No comments:

Post a Comment