Thursday, January 24, 2013

DHAMANA YA LULU YAPIGWA KALENDA

MAHAKAMA Kuu kanda ya  Dar es Salaam imebadilisha siku ya kusilizwa kwa maombi ya dhamana ya Mwigizaji nyota wa filamu nchini, Elizabeth Michael, maarufu kwa jina la Lulu,kutoka  Ijumaa ya kesho hadi Juma tatu ya January 28 mwaka huu.
 Lulu anashtakiwa kwa kosa la kumuua aliyekuwa msanii mwenzake wa fani hiyo, Steven Kanumba, bila kukusudia.
Taarifa za ndani kutoka Mahakamani hapo zilizolifikia tovuti ya Habarimpya.com na kudhibitishwa na vyanzo vya ndani kutoka Mahakamani hiyo zimedai kwamba msanii huyo anaweza kupata dhamana hiyo na kurudi uraiani huku akipangia tarehe nyingine ya kuwasilini Mahakamani hapo kwa ajili ya kesi hiyo.
Awali Lulu alikuwa akikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini baada ya upelelezi kukamilika alibadilishiwa mashtaka na kuwa ya kuua bila kukusudia, kisha kesi hiyo ikahamishiwa Mahakakama Kuu.

‘Hosteli za wanafunzi IFM Kigamboni sasa salama’


UONGOZI wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamazi wa Fedha (IFMSO) cha jijini Dar es Salaam, umesema hali ya usalama kwa sasa katika Hosteli za Kigamboni inaridhisha.
Waziri Mkuu wa IFMSO, Daniel Sarungi alisema jana kuwa tangu iundwe timu ya polisi inayoshirikiana na wanafunzi hao hali imekuwa tulivu kwa kipindi cha wiki moja iliyopita. Sarungi alisema kuwa hakujatokea uvamizi tena katika hosteli zao, lakini akaongeza kusema kuwa taarifa kamili ya ripoti ya timu hiyo itatolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Kuna amani sana, misako imefanyika lakini ripoti itatolewa Januari 30 na Kamanda Kova,” alisema Sarungi.
Kauli ya Kiongozi huyo wa wanafunzi haikutofautina na ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Englbert Kiondo, ambaye alisema taarifa inayohusu hali ilivyo itatolewa na Kamanda Kova.
Kwa upande wa wakazi wa Kigamboni, walisema kuwa wameshuhudia polisi wakifanya doria maeneo hayo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma kabla wanafunzi hawajaandamana.

Walisema pia wameona polisi wakiwakamata wahalifu kwenye maeneo hayo kutokana na misako wanayoifanya hali ambayo imeleta utulivu kwenye mji huo.
“Kwa sasa kumetulia inawezekana wanasikilizia (wahalifu), likini ingetakiwa polisi wawakamate wale vinara kwa sababu wanawafahamu” alisema Salum Rashid mkazi wa eneo hilo.
Naye mkazi mwingine anayejishughulisha na biashara ya kioski, alisema kuwa kumekuwa na utulivu kwani hata wanafunzi ambao ndiyo wateja wake wakubwa wanamwambia kuwa wanaweza kuacha vitu wakavikuta salama.
Eneo la Kigamboni lilikuwa  tete wiki iliyopita ambapo wanafunzi hao waliandamana kupinga vitendo vya udhalilishwaji walivyokuwa wakifanyiwa na wahalifu.
Wakati huohuo, Mwandishi Wetu Peter Edson anaripoti kuwa, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amesema ili kufanikisha mapambano dhidi ya uchafunzi wa mazingira jijini Dar es Salaam elimu ya usafi mabadiliko kifikra na kimtazamo vinatakiwa kwenda sambamba.
Akizindua kampeni ya usafi wa mazingira jijini Dar es Salaam Silaa alisema suala la usafi wa mazingira ni mtambuka hivyo ni lazima elimu ianze kutolewa mashuleni hadi vyuoni ili watu waweze kubadili fikra na mitazamo ya kudhani kuwa usafi unawahusu baadhi ya watu tu.
Alisema jiji likiwa safi magonjwa ya milipuko hayataweza kutokea lakini hivi sasa Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ukikumbwa sana na magonjwa ya mlipuko kwa sababu ya uchafunzi wa mazingira ulikithiri.
Naye meneja wa kampeni hiyo Elizabeth Stcheers alisema kwa sasa kampeni hiyo itahusisha kata tatu zilizopo katika Manispaa ya Ilala ambazo ni Kata ya kivukoni, Mchafukoge, na Kata ya Kisutu
Alisema huu ni mwanzo wa mpango ambapo baadaye zitahusishwa manispaa zingine katika Mkoa wa Dar es Salam lengo likiwa ni kuweka jiji safi na salama.


Source:Mwananchi

Tibaijuka atenganisha Mji wa Kigamboni na Temeke


WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ameanzisha Wakala wa Kuendeleza Mji wa Kigamboni (KDA). Kwa maana hiyo, mji huo hautakuwa tena chini ya mamlaka ya Manispaa ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Tibaijuka alisema Serikali imeamua kuanzisha wakala huo ili pamoja na mambo mengine, upange na kusimamia ujenzi wa mji wa kisasa katika eneo hilo.
“KDA imeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ya 1997 ili iweze kuhakikisha mji unajengwa na unakuwa bora,” alisema Profesa Tibaijuka.
Alisema kutokana na kuanzishwa kwa KDA, kata zote za Kigamboni, zitaungana na madiwani wake pamoja na mbunge wao watakuwa wakikutana katika Baraza la Ushauri la KDA.
“Kutakuwa na Baraza la Kigamboni ambalo madiwani na mbunge wao wataingia humo kujadili maendeleo ya mji huo na leo (jana), kutakuwa na kikao cha kwanza,” alisema Profesa Tibaijuka.

Alizitaja kata hizo kuwa ni Kigamboni, Tungi, Mjimwema, Vijibweni, Kibada, Pemba Mnazi, Kimbiji, Kisarawe II, Somangila, Kendwa, Sinda Chini na Sinda Juu.
Profesa Tibaijuka alisema eneo lote la Kigamboni lenye hekta 50,935, litaendelezwa na wananchi 80,000 wa eneo hilo watanufaika.

Profesa Tibaijuka alisema wananchi wa Kigamboni ambao wako kwenye maeneo ambayo yatahitajika kwa ajili ya ujenzi huo watashirikishwa ipasavyo katika mchakato mzima ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia zao kwa wakati.
Alisema fidia itatolewa kwa kila mwananchi na wahusika watahamishiwa katika maeneo mengine ndani ya mji huohuo wa Kigamboni, ili kupisha ujenzi.
“Mwananchi yeyote ambaye hatajisikia kubaki Kigamboni atalipwa fedha zake na kwenda kuishi kokote anakotaka iwe ni Kimara au Kibaha ataamua mwenyewe na tayari majengo ya kuwahamishia yameshaanza kujengwa,” alisema.
Profesa Tibaijuka alisema ni wakati wa Watanzania wanaoweza kuendeleza eneo la Kigamboni kujitokeza ili wapewe ‘blocks’ na kuondokana na suala la viwanja.
Alisema zaidi ya Sh11 trilioni zitatumika kujenga mji huo mpya ambao unatarajiwa kukamilika ifikapo 2032.

“Bajeti ya mwaka huu tulihitaji Sh600 bilioni, lakini tukapewa asilimia 10 ya fedha hizo ambayo ni Sh60 bilioni. Tunajipanga na hii ni moja ya mipango yetu kufanikisha ujenzi huo. Katika awamu ya kwanza tutahitaji kiasi cha Sh3 trilioni ili kuifanikisha.”
Mbunge hataki
Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile amepinga kuanzishwa kwa KDA na kueleza ni kuongeza gharama kwa Serikali akataka Manispaa ya Temeke iwezeshwe ili isimamie mji huo.

“Walishakuja na kutueleza hilo suala hata hivyo, sisi na manispaa tulikataa kwa kuwa uwezo wa kufanya kazi hiyo manispaa inayo hivyo hatuikubali mamlaka hiyo,” alisema Dk Ndugulile.
Aidha, alikanusha taarifa ya Profesa Tibaijuka kuwa angekutana nao katika mkutano wa Baraza jana akieleza kuwa hakuna mkutano kama huo kwa kuwa yeye na madiwani wenzake hawajataarifiwa.

Source:Mwananchi

Watu 5 wakatwa vichwa Maiduguri,Nigeria


Washukiwa wa kundi la kiisilamu wamewakata vichwa watu kadhaa mjini Maiduguri, Kaskazini mwa Nigeria.
Mtu mmoja ameambia BBC kuwa wanaume watano waliuawa wakati wa msako katika nyumba za watu usiku wa kuamkia leo.
Miongoni mwa walionyongwa ni baba na mwanawe.
Hata hivyo, jeshi la Nigerialimesema ni watu watatu pekee waliouawa.
Zaidi ya watu 20 sasa wamefariki katika mashambulizi tofauti, Kaskazini mwa Nigeria wiki hii pekee ambayo yanshukliwa kusababishwa na kundi la
Boko Haram pamoja na makundi mengine yanayotaka nchi hiyo kutumia sheria za kiisilamu.
Boko Haram wamelaumiwa kwa mauaji ya watu 23 katika mashambulizi tofauti Kaskazini mwa Nigeria.
Walio shuhudia mauaji hayo wanasema kuwa washambuliaji waliwalenga watu waliokuwa wanauza nyama ya wanyamapori, katika eneo la Damboa siku ya Jumatatu na kuwaua watu 18.
Watu wengine watano walifariki Jumanne wakati kundi la wanaume waliokuwa wanacheza mchezo wa kamari walishambuliwa mjini Kano.
Kundi la Boko Haram, linalopigana kutaka kuweka sheria za kiisilamu, nchini Nigeria limekuwa likifanya mashambulizi, katika sehemu kadhaa nchini humo.
Boko Haram imelaumiwa kwa vifo vya takriban watu 1,400, Kaskazini mwa Nigeria tangu mwaka 2010. Mwaka jana pekee , kundi hilo lilihusishwa na vifo vya watu 600.
Siku ya Jumatatu, watu waliokuwa wamejihami, walifyatulia risasi katika soko moja jimbo la Borno , wakiwalenga watu waliokuwa wanauza nyama ya nyani, na nguruwe.

Waisilamu wengi hawatumii kabisa nyama ya wanyama pori.
"watu waliokuwa wamejihami, na wanaoshukiwa kuwa wanachama wa kundi la Boko Haram, walikuja katika soko moja eneo hilo, na kuwapiga risasi watu 13, papo hapo na wengine watano walifariki kutokana na majereha yao.'' alisema afisaa mmoja.
Eneo la Damboa liko karibu na hospitali moja mjini Borno katika jimbo la Maiduguri, ngome ya Boko Haram.Kundi hilo liliundwa mjini humo mwaka 2002.
Wakati huohuo, ripoti zinasema kuwa shambulizi lengine baya sana limefanywa mjini Kano , mji mkuu Kaskazini mwa Nigeria,umbali wa kilomita 500, Magharibi mwa Damboa.
Watu waliokuwa wanaendesha pikipiki waliwanywaftulia risasi, vijana waliokuwa wanacheza nje , kwa mujibu wa taarifa za polisi.
Mchezo wa kamari pia umeharamishwa katika dini ya kiisilamu.

Wednesday, January 23, 2013

HAFLA ZA KUAPISHWA RAISI BARAK OBAMA

Rais Obama Akila kiapo

Rais Obama na mkewe Michelle akisalimia watu waliohudhuria hafla hiyo



obama na mkewe wakisakata dansi
Beyonce alikuwepo pia kuwatumbuiza watu waliofika kumpongeza Obama

wakiwa kenye dhifa aliyoandaliwa




Wapoteza maisha baada ya magari kuvaana uso kwa uso

WATU wawili wamefariki dunia baada ya magari mawili likiwamo la Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) kugongana uso kwa uso juzi usiku katika Barabara kuu ya Moshi-Himo.
Ajali hiyo ilitokea saa 2:00 usiku katika Kijiji cha Miwaleni Kata ya Kirua Vunjo, Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya gari la Kinapa Toyota Landcruicer kugongana na Toyota Corolla.
Dereva wa Toyota Corolla ambaye ni Fundi Makanika, Arcard Eligi alifariki dunia akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya KCMC wakati abiria katika gari la Kinapa, Ally Mohamed alikufa papo hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz alilithibitishia gazeti hili kuwapo kwa ajali hiyo lakini akasema hakuwa na taarifa kamili kwa kuwa alikuwa safarini kikazi mkoani Tanga.
Hata hivyo Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa), Erastus Lufungilo aliliambia gazeti hili kuwa abiria aliyekuwa katika gari la Hifadhi na kufariki dunia hakuwa mwajiriwa wa Kinapa.
“Ni ajali mbaya sana kwa sababu ukiangalia yale magari yalivyoisha (kuharibika) unaweza kupata picha hiyo, kishindo cha hiyo ajali ilikuwaje kwa kweli ni ajali mbaya,” alisema Lufungilo.
Lufungilo alisema dereva wa gari hilo la hifadhi pamoja na abiria katika gari dogo la binafsi lililogongana na gari la hifadhi, Harson Macha wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC.
Polisi wanachunguza chanzo cha ajali hiyo iliyotokea juzi saa 2:00 usiku.

Source:Mwananchi

SIKILIZA NGOMA MPYA YA IZZO BUSINESS FT QUICK ROCKA,NGWAIR-BALL PLAYER

Michu asaini mkataba mpya na Swansea

Mashambulizi wa Swanse Michu, amesaini mkataba mpya, na kuongeza muda wake na klabu hiyo kwa muda wa miaka minne ijayo.
Mchezaji huyo kutoka Uhispania, ameibuka kuwa miongoni mwa wachezaji bora wa ligi kuu ya Premier ya England tangu aliposajiliwa kwa kitita cha pauni milioni mbili nukta mbili na klabu ya Rayo Vallecano.
Michu mwenye umri wa miaka 26, sasa atasalia katika klabu hiyo hadi mwaka wa 2016.
Akiongea baada ya kusaini mkataba huo, Michu alisema, hakuwa na ugumu wowote kuongeza muda wake na Swanse.
Nyota huyo ambaye ana uwezo wa kucheza kama mcheza kiungo au mshambuliaji, amefunga magoli 16 baada ya kucheza mechi ishirini na nane.
Wachambuzi wa masuala ya soka nchini England wanasema kuwa kuwa yeye ni mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kusajiliwa na klabu hiyo ya Swansea.
Kocha wa Swansea, Michael Laudrup, amemsifu mchezaji huyo kwa mchango wake katika ufanisi wa klabu hiyo na kumtaja kama kito ya msimu.

FLAVIANA MATATA ASHINDA TUZO YA MWANAMITINDO BORA 2012


MWANAMITINDO wa kimataifa wa Tanzania, Flaviana Matata ameendelea kung’ara kimataifa baaada ya kushinda tuzo ya Nigeria’s Next Super model na kuwa mwanamitindo bora barani Afrika wa mwaka 2012 (Africa’s Most Outstanding  Model 2012).
Tuzo hiyo utolewa kwa wanamitindo ambao bado wanailetea sifa Afrika kimataifa na Flaviana amekuwa katika chati ya juu. Mwaka jana Desemba,  Flaviana alishinda tuzo nyingine  ya uwanamintindo bora kutoka kwa diaspora ya Waafrika.
Flaviana kwa ambaye kwa sasa anaishi na kufanya kazi ya uanamitindo New York nchini Marekani kupitia shirika la Wilhelmina Models, mpaka sasa ameweza kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na umahiri wake katika maonyesho ya mavazi.
Tangu ashinde taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2007, Flaviana amekuwa aking’ara katika kona zote za dunia na hasa baada ya kumaliza katika nafasi ya sita katika mashindano ya kimataifa ya Miss Universe, huku Tanzania ikishiriki kwa mara ya kwanza.

Ameweza kushiriki katika maonyesho ya mavaz mengi Ulaya na Amerika huku akitoa misaada mingi kwa Watanzania wenzake ambao wamekuwa na ndoto ya kufika mbali katika fani hiyo.

Kwa sasa Flaviana anaendesha taasisi yake, Flaviana Matata Foundation ambayo inasomesha watoto wa kike 16 na mwaka jana alitoa msaada wa vifaa vya kuokoa maisha kama sehemu ya kumbukumbu ya kuzama kwa meli ya MV Bukoba huku ikiwa kumbukumbu ya kifo cha mama yake mzazi katika ajali hiyo ya mwaka 1996.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Compass Communication Tanzania Limited, Maria Sarungi Tsehai alisema kuwa wamejisikia faraja sana kwa kumvumbua mwanamitindo huyo ambaye kwa sasa anashika chati ya juu Tanzania na nje ya nchi.

Maria alisema kuwa Flaviana amedhihirisha ubora wake na mpaka sasa amepitiliza kiwango cha kuitangaza Tanzania nje ya mipaka yake, ndoto ambayo alikuwa nayo muda mrefu.