Thursday, January 24, 2013

‘Hosteli za wanafunzi IFM Kigamboni sasa salama’


UONGOZI wa Serikali ya wanafunzi wa Chuo cha Usimamazi wa Fedha (IFMSO) cha jijini Dar es Salaam, umesema hali ya usalama kwa sasa katika Hosteli za Kigamboni inaridhisha.
Waziri Mkuu wa IFMSO, Daniel Sarungi alisema jana kuwa tangu iundwe timu ya polisi inayoshirikiana na wanafunzi hao hali imekuwa tulivu kwa kipindi cha wiki moja iliyopita. Sarungi alisema kuwa hakujatokea uvamizi tena katika hosteli zao, lakini akaongeza kusema kuwa taarifa kamili ya ripoti ya timu hiyo itatolewa na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova.
“Kuna amani sana, misako imefanyika lakini ripoti itatolewa Januari 30 na Kamanda Kova,” alisema Sarungi.
Kauli ya Kiongozi huyo wa wanafunzi haikutofautina na ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Temeke, Englbert Kiondo, ambaye alisema taarifa inayohusu hali ilivyo itatolewa na Kamanda Kova.
Kwa upande wa wakazi wa Kigamboni, walisema kuwa wameshuhudia polisi wakifanya doria maeneo hayo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma kabla wanafunzi hawajaandamana.

Walisema pia wameona polisi wakiwakamata wahalifu kwenye maeneo hayo kutokana na misako wanayoifanya hali ambayo imeleta utulivu kwenye mji huo.
“Kwa sasa kumetulia inawezekana wanasikilizia (wahalifu), likini ingetakiwa polisi wawakamate wale vinara kwa sababu wanawafahamu” alisema Salum Rashid mkazi wa eneo hilo.
Naye mkazi mwingine anayejishughulisha na biashara ya kioski, alisema kuwa kumekuwa na utulivu kwani hata wanafunzi ambao ndiyo wateja wake wakubwa wanamwambia kuwa wanaweza kuacha vitu wakavikuta salama.
Eneo la Kigamboni lilikuwa  tete wiki iliyopita ambapo wanafunzi hao waliandamana kupinga vitendo vya udhalilishwaji walivyokuwa wakifanyiwa na wahalifu.
Wakati huohuo, Mwandishi Wetu Peter Edson anaripoti kuwa, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amesema ili kufanikisha mapambano dhidi ya uchafunzi wa mazingira jijini Dar es Salaam elimu ya usafi mabadiliko kifikra na kimtazamo vinatakiwa kwenda sambamba.
Akizindua kampeni ya usafi wa mazingira jijini Dar es Salaam Silaa alisema suala la usafi wa mazingira ni mtambuka hivyo ni lazima elimu ianze kutolewa mashuleni hadi vyuoni ili watu waweze kubadili fikra na mitazamo ya kudhani kuwa usafi unawahusu baadhi ya watu tu.
Alisema jiji likiwa safi magonjwa ya milipuko hayataweza kutokea lakini hivi sasa Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ukikumbwa sana na magonjwa ya mlipuko kwa sababu ya uchafunzi wa mazingira ulikithiri.
Naye meneja wa kampeni hiyo Elizabeth Stcheers alisema kwa sasa kampeni hiyo itahusisha kata tatu zilizopo katika Manispaa ya Ilala ambazo ni Kata ya kivukoni, Mchafukoge, na Kata ya Kisutu
Alisema huu ni mwanzo wa mpango ambapo baadaye zitahusishwa manispaa zingine katika Mkoa wa Dar es Salam lengo likiwa ni kuweka jiji safi na salama.


Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment