WATU wawili wamefariki dunia baada ya magari mawili likiwamo la
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) kugongana uso kwa uso
juzi usiku katika Barabara kuu ya Moshi-Himo.
Ajali hiyo ilitokea saa 2:00 usiku katika Kijiji
cha Miwaleni Kata ya Kirua Vunjo, Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya gari
la Kinapa Toyota Landcruicer kugongana na Toyota Corolla.
Dereva wa Toyota Corolla ambaye ni Fundi Makanika,
Arcard Eligi alifariki dunia akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya
KCMC wakati abiria katika gari la Kinapa, Ally Mohamed alikufa papo
hapo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz
alilithibitishia gazeti hili kuwapo kwa ajali hiyo lakini akasema hakuwa
na taarifa kamili kwa kuwa alikuwa safarini kikazi mkoani Tanga.
Hata hivyo Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro
(Kinapa), Erastus Lufungilo aliliambia gazeti hili kuwa abiria aliyekuwa
katika gari la Hifadhi na kufariki dunia hakuwa mwajiriwa wa Kinapa.
“Ni ajali mbaya sana kwa sababu ukiangalia yale
magari yalivyoisha (kuharibika) unaweza kupata picha hiyo, kishindo cha
hiyo ajali ilikuwaje kwa kweli ni ajali mbaya,” alisema Lufungilo.
Lufungilo alisema dereva wa gari hilo la hifadhi
pamoja na abiria katika gari dogo la binafsi lililogongana na gari la
hifadhi, Harson Macha wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa KCMC.
Polisi wanachunguza chanzo cha ajali hiyo iliyotokea juzi saa 2:00 usiku.
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment