Umoja
wa Mataifa UN umetaka kumalizwa mara moja kwa ufadhili unaofanywa kwa Makundi
ya Waasi ya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC unaofanywa na mataifa
jirani kitu kinachochangia kuendelea na vita Mashariki mwa Taifa hilo. Kauli
hiyo imetolewa kwenye mkutano uliotishwa Jijini New York katika makao Makuu ya
Umoja wa Mataifa UN ukiwa na dhamira ya kuangalia mbinu zinazofaa ili kumaliza
machafuko yanayoendelea Mashariki mwa DRC kwa muda sasa. Waziri wa Mambo ya Nje
wa Marekani John Kerry ambaye aliongoza mkutano huo amesema wakati umefika sasa
kwa mataifa yanayofadhili Kundi la Waasi la M23 waache kufanya hivyo mara moja
kitu kitakachosaidia kupatikana kwa amani.
Kerry aliuambia mkutano wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC nchi yake imekuwa ikisitikishwa na taarifa za
Kundi la Waasi la M23 kuendelea kupatiwa ufadhili kutoka kwa nchi jirani na
DRC.
Waziri huyo wa mambo ya Nje ambaye
alikuwa Rais wa Mkutano huo amesema wakati umefika kwa pande zinazolifadhili
Kundi la Waasi la M23 kijeshi kuacha kufanya hivyo kwa kuwa wanaushahidi
unaothibitsha madai hayo.
Mkutano huo wa Baraza la Usalama la
Umoja wa Mataifa UNSC uliwaleta pamoja wanachama kumi na tano wa kudumu pamoja
na Rwanda lengo likiwa ni kuhakikisha mkakati madhubuti unakuwepo kumaliza vita
vya Mashariki mwa DRC.
Uingereza, Ufaransa na Mataifa mengine
wameungana na Kerry kutaka ufadhili wowote wa kijeshi kwa Kundi la Waasi la M23
usitishwe mara moja kwa ajili ya mustakabali mwema wa eneo la Ukanda wa Maziwa
Makuu ICGLR.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN Ban
Ki Moon ametoa wito kwa pande zote yaani Serikali ya Kinshasa na Waasi wa M23
kurejea kwenye meza ya mazungumzo huko Kampala yanayosimamiwa na ICGLR.
Ban amekiri mazungumzo ni moja ya njia
muafaka kabisa kumaliza mapigano yanyoendelea kushuhudiwa Mashariki mwa DRC
kati ya jeshi la Serikali la FARDC na Kundi la Waasi la M23.
Naye Mjumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa katika eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu ICGLR Mary Robinson amekiri hatua
ya kuendelea kufadhiliwa kwa Kundi la M23 inasikitisha na kuchochea machafuko
zaidi.
Rwanda imekuwa ikinyooshewa kidole cha
lawama kwa kuwasaidia Waasi wa M23 kupambana na Jeshi la FARDC na imesisitiza
yenyewe inalengo la dhati kuhakikisha utulivu unakuwepo nchini DRC.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise
Mushikiwabo amesema utulivu wa taifa hilo unategemea zaidi hali ya usalama
katika nchi jirani ya DRC hivyo wao wanaunga mkono juhudi zinazochukuliwa
kumaliza vita hivyo.
No comments:
Post a Comment