Marekani inaendelea
na mpango wake wa kutoa ndege za kivita kwa jeshi la Misri licha ya msukosuko
wa kisiasa unaokumba nchi hiyo. Hatua hii inajiri wakati Marekani ikiendelea
kutathmini matukio ya wiki jana ambapo jeshi lilimuondoa madarakani Rais
Mohammed Morsi.
Msaada wa kijeshi kwa
Misri ungesitishwa endapo Marekani ingelitaja matukio ya wiki jana kama
mapinduzi ya kijeshi. Kundi la Muslim Brotherhood linalomuunga mkono Morsi
linasisitiza arejeshwe madarakani
Wafuasi wake wamekua wakiandamana karibu na
kambi kuu ya jeshi ambapo anaaminika kuuzuiliwa. Hapo Jumatatu,wafuasi wa
Brotherhood 51 waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi wakati wanakabiliano.
Utawala wa mpito umesema kwamba Bw. Morsi
anazuiliwa eneo salama na kwamba haki zake zinazingatiwa.Maafisa wa Marekani
wamesema ndege mpya za kivita aina ya F-16 zitawasilishwa katika wiki chache
zijazo.
Mpango wa kufadhili jeshi ulianza kutekelezwa
mapema mwaka huu na jeshi inatarajia kupokea ndege 20 za kivita. Msemaji wa
ikulu ya Rais amesema Marekani haitabadilisha mpango wa kufadhili jeshi la
Misri, japo inaendelea kutathmini kuhusu matukio ya kisiasa. Msaada wa kijeshi
nchini Misri ambao hutolewa na Marekani hufikia dola bilioni 1.3 kila mwaka.
Hapo Jumanne, kibali cha kumkamata kiongozi wa
Muslim Brotherhood Mohamed Badie kilitolewa pamoja na wakuu wengine tisa wa
kundi hilo. Viongiozi hao wamelaumiwa kwa kuchochea ghasia mjini Cairo ambapo
zaidi ya watu 50 waliuawa na mamia kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment