Dar es Salaam. Katika kuhakikisha haifanyi makosa zaidi, klabu ya Simba juzi iliwasainisha wachezaji watatu, Sino Agustino, Marcel Kaheza ‘Rivaldo’ na Omary Salum ‘Inzagi’.
Sino ni mshambuliaji amesajiliwa na Simba akitokea Prisons ya Mbeya kwa mkataba wa miaka miwili, ambapo mshambuliaji Malceli na beki wa kushoto Omary wamepandishwa kutoka Simba B.
Wachezaji hao wakisaini kwenye ofisi za Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ Sinza jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia usajili huo, Itang’are alisema,”Katika kuhakikisha hatufanyi makosa tumemalizana na wachezaji hawa kwa lengo la kuiboresha timu katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.”
Alisema,”Tumewasajili vijana hawa baada ya kufanya majaribio na makocha wameridhika na viwango vyao kwa kipindi chote cha majaribio,”alisema Itang’are.
Naye, Sino akizungumzia kusajiliwa na Simba alisema amefurahishwa na benchi la ufundi la Simba kwa kumwamini na kumjumuisha kikosini hapo, hivyo ameahidi kuifanyia kazi nzuri klabu hiyo ya mtaa wa Msimbazi.
“Nashukuru kuchaguliwa Simba, nawaahidi mashabiki nitawafanyia kazi nzuri, kikubwa naomba ushirikiano wao,”alisema Sino.
Naye Malcel alisema,” Nimefurahi kusajiliwa Simba na sasa najipanga kuhakikisha naifanyia mazuri klabu hii kwenye ligi na mashindano mengine yatakayotukabiri.”
Kwa upande wa Omary yeye alisema atajitoa kwa nguvu zote kuifanya Simba ing’are.
Tayari Simba imempa mkataba tena Amri Kiemba, imemsajili beki Samwel Senkoon raia wa Uganda kutoka URA, imemsajili Andrew Ntala kutoka Kagera Sugar, Ibrahim Twaha ‘Messi’ kutoka Coastal Union ya Tanga na wengine wa timu B kama Ramadhani Singano ‘Messi’, Hassan Khatib na Edward Christopher.
Katika hatua nyingine, Simba iliifunga timu ya Kiluvya bao 1-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam.
Bao hilo la Simba lilifungwa na Sino kutokana na pasi ya Malcel.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment