Thursday, July 25, 2013

IGP Mwema, Tendwa wakamia CHADEMA

JESHI la Polisi nchini na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, wanaonekana kuanza mkakati maalumu wa kukidhoofisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwaandama viongozi wake kuhusu ushahidi wa mlipuko wa bomu jijini Arusha na mpango wa kutaka kuanzisha kambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana kwa ajili ya ulinzi.
Kutokana na mlipuko huo wa bomu Juni 15 mwaka huu, eneo la Soweto jijini Arusha ulioua watu wanne na kujeruhi wengine zaidi ya 60 katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani, CHADEMA ilitangaza kuanza mpango wa kutoa mafunzo kwa vijana wake kwa ajili ya kulinda mikutano na viongozi wake.
Hata hivyo, msimamo huo wa CHADEMA ulitafsiriwa tofauti na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jeshi la Polisi linaloongozwa na IGP Said Mwema, na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa wakidai hatua hiyo ni kinyume cha sheria za nchi, katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
Kauli hizo zilipokelewa kwa mtazamo tofauti na wadau wa siasa nchini wakihoji jeshi hilo na Tendwa walikuwa wapi kwa kutoionya CCM yenye kikundi cha vijana cha Green Guard ambacho kinapewa mafunzo ya kijeshi kwa ajili ya shughuli za chama.
Licha ya vyombo vya habari kuonyesha picha kadhaa za mafunzo ya kikundi hicho cha CCM kikiwa na vijana wenye silaha, polisi na Tendwa wamekuwa na kigugumizi cha kuzungumzia jambo hilo badala yake wameendelea kuwatisha viongozi wa CHADEMA kuachana na mpango huo.
Katika suala hilo, Tendwa amekuwa na kauli za kujikanganya huku naye akikwepa kuizungumzia Green Guard wakati viongozi waandamizi wa polisi nao wamekuwa na ndimi mbili zinazokinzana kwenye suala hilo ambalo wamelibebea bango wakitaka kufifisha tukio la mlipuko wa Arusha.
Jumamosi iliyopita, gazeti hili lilichapisha barua iliyoandikwa na ofisi ya Tendwa kwenda kwa CHADEMA yenye kumb. Na RPP/CHADEMA/72/32 ikikiruhusu chama hicho kuanzisha vikundi vya ulinzi na usalama kama ilivyo katika katiba yao.
Ofisi hiyo ya msajili kupitia kwa Naibu Msajili, Sisty Nyahoza, jana ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikikana kuwahi kutoa ruhusa kwa CHADEMA au chama chochote cha siasa kufanya mafunzo ya ukakavu au mafunzo ya kutumia nguvu ya aina yoyote kwa wanachama wake au mtu yeyote.
Hata hivyo, katika hali ya kuonyesha kuwa Tendwa anaibeba CCM, licha ya kutoa vitisho kwa CHADEMA kuwa atawachukulia hatua za kisheria endapo watashindwa au kukataa kutii agizo la kutoanzisha makambi hayo, hakusema chochote kwa chama tawala ambacho kinaendesha kambi za kujihami.
Julai 9 mwaka huu, CHADEMA kupitia kwa Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, walisema kufuatia mlipuko wa bomu Arusha, chama hicho kinakusudia kuanzisha kambi za mafunzo kwa vijana watakotumika kulinda viongozi katika shughuli zake kutokana na Jeshi la Polisi kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Siku chache baadaye, Mbowe alivamiwa usiku wa manane nyumbani kwake na askari kadhaa wakidai kuwa walitaka awapatie ushahidi wa video ya mauaji aliyodai kuwa nayo ikiwaonyesha baadhi ya polisi walivyoshiriki kwenye tukio la mlipuko wa bomu Arusha.
Baada ya Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kufichua tukio hilo kwenye mkutano wa hadhara kesho yake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alidai hana taarifa za askari wake kufika nyumbani kwa Mbowe kumkamata.
Jeshi hilo kisha liligeuza hoja na kumtaka Mbowe ajisalimishe kwa ajili ya mahojiano kuhusu kauli yake ya kuhusu chama kutaka kuanzisha makundi ya mafunzo ya ukamamavu kwa vijana wao.
Julai 17 mwaka huu, Mbowe aliandikiwa barua akiamrishwa awasilishe ushahidi wa video aliyodai kuwa nayo, ikiwaonyesha baadhi ya polisi walivyoshiriki kwenye tukio la mlipuko wa bomu Arusha.
Wakati Mbowe akiamriwa kufanya hivyo kabla ya juzi saa nane mchana, jeshi hilo halijawahi kuwahoji Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ambao walinukuliwa wakidai wana ushahidi kwamba CHADEMA walijilipua wenyewe.
Juni 20 mwaka huu, Mkuu wa Mafunzo na Operesheni wa jeshi hilo, Paul Chagonja aliwaeleza wanahabari kuwa Mbowe anapaswa kuwa mkweli na kuacha kuuchezea umma kwani alichowaeleza polisi ni tofauti akisema hana ushahidi huo wa mlipuko wa bomu bali alielezwa na wafuasi wake.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Chagonja huyo huyo ndiye amemwamuru Mbowe tena kupeleka ushahidi huo polisi akitamba kuwa baada ya kukaidi kufanya hivyo, polisi inao makachero wake wanaojua jinsi gani ya kuendelea na kazi hiyo.
Muda aliopewa Mbowe umemalizika bila kuwasilisha ushahidi huo, akidai kuwa hawezi kwenda kinyume na msimamo wa chama kwani walikwishamwandikia Rais Jakaya Kikwete, wakimtaka aunde tume huru ya majaji ndipo watapeleka ushahidi wao huo na mwingine.
Mbowe alisema kuwa jeshi hilo ni watuhumiwa, hivyo kamwe hawawezi kupeleka ushahidi huo kwao, na kukitaka chombo hicho cha dola kufungua kesi mahakamani ili CHADEMA wapeleke ushahidi huo huko.
Jana, Mbowe alijisalimisha tena polisi kama alivyokuwa ameamriwa, lakini hakupeleka ushahidi huo, na jeshi hilo lilimwamuru tena kupeleka ushahidi huo kwa maandishi Ijumaa wiki hii.


source:Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment