![]() |
Mwenyekiti wa Tume huru ya Uchaguzi Nchini Zimbabwe Bi Joyce Kazembe |
ZEC imesema zoezi hilo la utoaji
wa vitambulisho kwa waangalizi linakwenda sanjari na kutoa huduma kama hiyo kwa
waandishi wa habari ambao watakuwepo nchini Zimbabwe kwa ajili ya kukusanya
habari wakati wa uchaguzi na baadaye ya uchaguzi.
Makamu Mwenyekiti wa ZEC Joyce
Kazembe akizungumza na waandishi wa habari pamoja na waangalizi hao amesema
hadi sasa wameshatoa vitambulisho 18,000 kwa waangalizi wa ndani na
vitambulisho 1,500 kwa waangalizi kutoka nje.
Kazembe amesema zoezi hilo
lingali linaendelea na litafungwa rasmi siku nne kabla ya kufanyika kwa
uchaguzi huo uamuzi ambao umetolewa kwa kuwa Tume Huru ya Uchaguzi ZEC inataka
ijue kabisa idadi ya vitambulisho ilivyotoa.
Tume Huru ya Uchaguzi ZEC imesema
waangalizi ambao wamepewa vitambulisho hivyo watakuwa na ruhusa ya kuangalia
kile kitakachokuwa kinafanyika kwenye vituo 9,650 vya kupigia kura
vitakavyokuwa kwenye kata 1,958 nchi nzima.
ZEC imesema pia kila Ubalozi
ambao upo nchini Zimbabwe umepewa nafasi zisizozidi tano za waangalizi wake
huku pia Mashirika yote yasiyo na Kiserikali yakipewa fursa ya kufanya
uangalizi pamoja na makanisa kutoka majimbo kumi.
Makamu Mwenyekiti wa ZEC
amethibitisha hadi kufika sasa wameshatoa vitambulisho 294 kwa waandishi wa
habari wa ndani huku waandishi 28 kutoka nje nao wakipewa ruhusa hiyo ya
kuripoti uchaguzi huo.
Tume Huru ya Uchaguzi imeendelea
kusisitiza waangalizi kutoka nchini Marekani na mataifa wanachama ya Umoja wa
Ulaya EU hawataruhusiwa kushiriki kwenye zoezi hilo kutokana na wao kuiwekea
vikwazo Zimbabwe.
Waangalizi ambao wameshawasili
nchini Zimbabwe ni kutoka Umoja wa Afrika AU, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika SADC, COMESA pamoja na wengine ambao ni Mashirika yasiyo ya
Kiserikali.
Uchaguzi Mkuu nchini Zimbabwe
umepangwa kufanyika tarehe 31 mwezi Julai ambao kinyang'anyiro kikali
kinatarajiwa kuwa kati ya Rais Robert Gabriel Mugabe anayetetea wadhifa wake
dhidi ya Mpinzani wake Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai.
No comments:
Post a Comment