Friday, November 30, 2012

SENEGAL WAPIGWA FAINI

Shirikisho la Soka Barani Afrika limeipiga marufuku Senegal isitumie uwanja wa Leopold Sedar Senghor, Dakar, kwa michuano ya kimataifa kwa kipindi cha mwaka mmoja kama adhabu ya vurugu iliyotokea wakati wa mechi mnamo mwezi Oktoba.
Shirikisho la Kandanda la Senegal pia lilipigwa faini ya dola za Kimarekani 100,000 kwa vurugu zilizofanywa na makundi ya mashabiki baada ya mchuano wa mchujo wa kuwania Kombe la Afrika dhidi ya Ivory Coast.
Sasa itabidi timu hiyo ya Simba wa Teranga  itafute kiwanja kingine kwa ajili ya michuano ya mchujo itakayofanyika mwaka ujao ya Kombe la Dunia 2014. Watacheza na Angola, na Uganda.
Mnamo 2007 Togo iliadhibiwa baada ya mashabiki wao kuzua fujo baada ya kutupwa nje ya mchuano wa Kombe la Afrika la 2008 na wageni Mali.
Iliibidi Togo icheze michuano mitatu iliyofuatia katika kiwanja ambacho kilikuwa hakihusishwi na upande wowote, na ikapigwa marufuku kucheza katika kiwanja cha kimataifa kwa muda wa miezi sita.

No comments:

Post a Comment