Wednesday, February 20, 2013

Mbowe: Sasa tumekuja kivingine

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeanza kubadili muundo wake, na kutekeleza wa sera yake ya majimbo.
Juzi chama hicho kilizindua jimbo la Kanda ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.
Uzinduzi wa Kanda hiyo umefanyika Jijini Arusha ambapo mbunge wa Karatu, Israel Natse ameteuliwa kuwa Mwenyekiti huku Amani Golugwa akiwa Katibu wake.
Katika mahojiano na gazeti hili, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe amefafanua mikakati, malengo na sera hiyo akisema hailengi kujitenga wala kugawa nchi kama inavyodaiwa “waliofilisika kisera na kisiasa”.
“Kuwa na Kanda siyo kujitenga, bali ni kusogeza mfumo na shughuli za chama kila sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala ya mtindo uliozoeleka wa kila kitu kuendeshwa kutokea Dar es Salaam,” anafafanua Mbowe.
Mwenyekiti huyo ambaye ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, anasema Sera ya Kanda siyo ukabila, akitolea mfano Kanda ya Kaskazini inayoundwa na watu wa makabila zaidi 25 wenye imani na dini tofauti.
Anasema sera hiyo itawezesha wanachama wa Chadema waliotapakaa kila sehemu nchini kupata fursa ya kuonyesha na kutumia vipaji na uwezo wao wa uongozi katika harakati za kukijenga chama hicho kikuu cha upinzani.
Anasema mfumo huo utaondoa dhana kuwa Chadema ni Mbowe, Dk Willibrod Slaa, Zitto Kabwe, Godbless Lema, John Mnyika na wengine wachache wenye majina kitaifa, badala yake kila mwanachama atatumia kipaji na uwezo wake pale alipo kukijenga na kukieneza Chadema.
“Kinachotuunganisha na ambacho tunakisimamia kama chama cha siasa ni Utaifa wetu, umoja, mshikamano na heshima kwa kila mtu bila kujali dini, imani wala kabila lake,” anasisitiza
Kanda zingine na mikoa inayoziunda kwenya mabano ni Mashariki (Dar es Salaam na Pwani), Kusini (Lindi na Mtwara, Kati (Morogoro, Dodoma na Singida), Nyanda za Juu Kusini (Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma) na Magharibi inayoundwa na mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma na Tabora.
Kanda zingine ni Ziwa Mashariki (Shinyanga, Simiyu na Mara), Ziwa Magharibi (Mwanza, Geita na Kagera), Pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba) na Unguja (Mjini Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja).
Mbowe anasema utekelezaji wa sera na mfumo wa Kanda kutaiwezesha Chadema kutumia mbinu anazoziita za medani kwa kushambulia kwa kushtukiza kutoka kila kona bila ‘askari’ wake kujulikana.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment