WANACHAMA wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) wa mkoani Simiyu,
wilaya ya Meatu wamesema mfuko huo pamoja na kutokuwa na tija kwao ni
sawa mnyanganyi anayewanyang’anya sehemu ya mishahara yao kwa njia ya
udanganyifu.
Wakazi wa maeneo mbalimbali ya wilayani humo,
wanaeleza kusikitishwa kwao na kitendo cha kukatwa mishahara yao mara tu
wanapoajiriwa, kwa maelezo kuwa wanakuwa wamejiunga na NHIF bila hata
kuhojiwa ikiwa wapo tayari kujiunga na mfuko huo au la.
Tatizo kubwa zaidi linaelezwa kuwa ni kukatwa
fedha hizo zinazoelezwa kutumika kugharamia huduma za matibabu ya
mwajiriwa na wanafamilia wake wasiozidi wanne, lakini imebainishwa kuwa
wahusika hawapati huduma hizo kutokana na kutokuwa na kadi za uanachama
na hivyo, mbali na kukatwa mishahara bado hujikuta wakitoa fedha taslimu
kugharamia huduma hizo pindi wanapougua.
Paul Nlimandago (42) mkazi wa Majengo alisema
mshahara wake ulikuwa ukikatwa michango ya mfuko huo kwa kipindi cha
miaka minne huku yeye na familia yake wakipata huduma za afya kwa kulipa
fedha taslimu, kutokana na kutopatiwa kadi za uachama.
“Nilipata kadi ya uanachama miaka minne tangu
mshahara wangu ulipoanza kukatwa michango ya uanachama…, nilikuwa najaza
fomu, napeleka picha na fedha zinakatwa kila mwezi kwa kipindi chote
hicho bila kupata kadi,” anabainisha Nlimandago
Naye Juma Said (43) anabainisha kuwa wanachama
hawana imani na mfumo unaotumika kulipia gharama wanazotumia, kwani
hutakiwa kuweka sahihi ambazo hazioneshi kiasi cha fedha kitakachodaiwa
na watoa huduma, kwa ajili ya malipo ya huduma.
“Bima ya afya ni wizi mtupu, mtu unatibiwa kisha
unapewa makaratasi usaini huku gharama unazodaiwa kutokana na huduma
uliyopatiwa zikiwa hazioneshwi; hii siyo sawa, nashauri fomu ambazo
wanachama tunasaini baada ya kuhudumiwa zirekebishwe, iwekwe sehemu
ambayo mtu utaona deni lako ili uidhinishe malipo unayoafiki kuyatumia,”
Said anaeleza na kushauri.
Anasema jambo la kusikitisha zaidi ni mtu kutakiwa
kusaini karatasi ambayo haufahamu wataenda kudai kiasi gani cha fedha
kisha unaelezwa, “dawa ulizoandikiwa zote hazipo, nenda ukanunue nje.”
anasema inaumiza na kukatisha tamaa kuliko maana inayopatikana katika
neno sana.
Shaban Alley (40) anashauri mamlaka husika
zifuatilie kwa karibu huduma wanazopatiwa wanaochangia malipo ya huduma
za afya, kwa kufanya uchunguzi wa kushtukiza na kwamba wanaotakiwa
kutekeleza jukumu hilo ni wasioishi eneo linalochunguzwa, ili kuondoa
uwezekano wa kufichiana dhambi na kulindana.
“Wakitaka wapate ukweli, wanatakiwa wafike ghafla
bila kutoa taarifa na kujifanya wagonjwa wenye kadi za kuchangia huduma
za afya kupitia NHIF au CHF, wakihitaji kuhudumiwa hata kwenye
hospitali binafsi ambazo zina mikataba na NHIF; watashuhudia jinsi
wanachama wao wanavyopata shida mbalimbali wanapohitaji huduma hizo,”
anaeleza Alley
Greyson Kakulu, mwanachama mwingine wa NHIF
anapotakiwa kuzungumzi hali ya huduma za afya akiwa katika mpango huo wa
kulipia huduma za afya kabla ya kuugua anasema: “Siridhishwi hata
kidogo ni mwaka wa tatu sasa tangu nijiunge na mfuko huu, kila mwezi
mshahara wangu unakatwa lakini sihudumiwi kama mwananchama kwa sababu
sina kadi,”anaeleza na kuongeza:
“Nagharamia huduma za afya ninazopatiwa mimi na
familia yangu lakini ninapokwenda kudai kurejeshewa fedha zangu sijawahi
kurudishiwa; hali hii inaumiza sana, hasa ikizingatiwa mtu huwezi
kukataa kujiunga wala kujitoa, naomba ishughulikiwe.”
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment