Tuesday, February 12, 2013

PAPA BENEDICT AJIUZULU NAFASI YAKE



Huko Ujerumani, msemaji wa serikali amesema kuwa anaheshimu kazi kubwa iliyofanywa na Papa huyu aliyezaliwa katika Jimbo la Bavaria la nchini humo.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, amemsifu Papa kwa jitihada zake za kuimarisha mahusiano baina ya Vatican na Uingereza.
Askofu mkuu wa Canterbury amesema amazipokea taarifa za kujiuzulu kwa Papa kwa huzuni kubwa ingawa anaelewa undani wa hatua yake.
Kiongozi wa Ujeremani, Bi. Angela Merkel amesifu mchango wa Papa wa kupendekeza mjadala baina ya makanisa, waislamu na wayahudi.
Alikumbusha hotuba ya Papa alipozuru bunge la Ujerumani mnamo mwaka 2011.
Uwamuzi na hatua ya Papa Benedict XVI wa kujiuzulu mwishoni mwa mwezi huu baada ya takriban miaka minane akiongoza Kanisa Katoliki kwa hoja kuwa umri wake wa miaka 85 ni mkubwa kiasi kwamba hawezi kuendelea kuhudumu zaidi ya umri huo.
Makao makuu ya Kanisa Katoliki huko Vatican yanasema yanatarajia Papa mpya atachaguliwa kabla ya mwisho wa mwezi wa tatu, na sherehe za Pasaka.
Tabia ya kujiuzulu kwa Papa si ngeni, ingawa ni tukio jipya katika karne za hivi karibuni.
Msemaji wa Vatikani Father Federico Lombardi, amesema kuwa hata wasaidizi wa Papa wa karibu mno hawakuwa na fununu juu ya tukio hili.
Kaka wa Papa huyu mzaliwa wa Ujerumani alipewa ushauri na Daktari wake asifanye ziara nyingine yoyote ya Marekani na kwamba kwa miezi kadhaa Mtakatifu Papa amekuwa akitafakari kujiuzulu.
Akizungumza kutoka nyumbani kwake huko Regensburg, Ujerumani, Georg Ratzinger amesema kuwa Kaka yake alikuwa ameanza kupata shida ya kutembea na kwamba kujiuzulu kwake ni hatua ya kimaumbile.
Wakati wa kutawazwa kama Papa, Kadinali Joseph Ratzinger alikuwa mmojawapo wa mapapa wapya kuchaguliwa akiwa mwenye umri mkubwa wa miaka 78.
Alitangazwa Papa mnamo mwezi Aprili 2005 kufuatia kifo cha marehemu John Paul wa pili.
Uongozi wake ulitokea wakati wa wimbi kali la ubakaji kulikumba kanisa katoliki katika kipindi cha miongo mingi, ubakaji uliofanywa na watawa dhidi ya watoto wavulana.
Katika taarifa yake, Mtakatifu Papa amesema: "baada ya kujichunguza binafsi na nafsi yangu mbele ya Mola wangu, nimefikia uwamuzi kuwa uwezo wangu na afya, ukiambatana na umri mkubwa, ni mambo yatakayokwaza jitihada zangu za kuendelea kuliongoza Kanisa Katoliki.
Kuna kipengele katika sheria ya Kanisa kinachosema kuwa kujiuzulu kwa Papa kunakubalika iwapo kitendo hicho kimefanywa kwa hiari na kwa utaratibu unaostahiki.

No comments:

Post a Comment