Thursday, February 14, 2013

Ofisa usalama mbaroni wizi kontena

VIGOGO watano akiwamo Ofisa wa Usalama wa Taifa wanashikiliwa polisi, kwa tuhuma za kutaka kusafirisha kontena la madini aina ya Tantalite yenye thamani ya Dola 22,000 za Marekani yaliyokuwa  yakisafirishwa nje ya nchi.
Akizungumza na Dar es Salaam jana, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliapa kuilinda Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa udi na uvumba.
Kiapo hicho alikitoa jana wakati akiwataja watu  wanaoshikiliwa na polisi kwa kuichafua TPA,  wakati yeye akifanya jitihada za kuisafisha.
Aliwataja watu hao  kuwa ni Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mmiliki wa Kampuni ya Uwakala wa Kusafirisha Mizigo ya GFC na msaidizi wake.
Wengine ni  Ofisa wa Mamlaka ya Ukaguzi Madini (TMAA),  Mmiliki wa Bandari Kavu na Ofisa wa Usalama  wa Taifa.
Dk Mwakyembe alisema mzigo huo uliokamatwa ukitaka kusafirishwa kwenda nje ya nchi,  madini yake aina ya Tantalite hayapatikani nchini, bali nchi za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alisema walibaini katika nyaraka  zinazohusiana na kusafirishwa kwa madini hayo kuwa, zinaonyesha madini hayo yanatoka nchini wakati siyo kweli.
Kuhusu Ofisa wa Usalama wa Taifa, Mwakyembe alisema ni mtu muhimu ambaye taifa linamwamini kuficha siri za nchi, lakini akashangaa kuwamo kwenye mlolongo huo.
“Yaani sisi tunafanya kazi ya kuisafisha bandari, watu hawa wanaichafua kuifanya kuonekana ni uchochoro wa kusafirisha magendo,” alisema Dk Mwakyembe na kuongeza:
“Kutokana na hili, kampuni mbili za meli za Safmaline na Maikesi zimesitisha kusafirisha mizigo yao, kutokana na michezo michafu kama hii, watu siyo waaminifu wanabadilisha mizigo halisi  kama madini wao wanaweka simenti au magadi ambayo yana uzito sawa na mzigo halisi.”
Aliongeza kuwa mmiliki wa Bandari Kavu ya PMM na mtendaji wake mkuu nao pia wanahojiwa  polisi kutokana na tuhuma hizo.
Kuhusu mfanyakazi wa TRA, Dk Mwakyembe alisema ndiye aliyetoa ridhaa ya mzigo huo kusafirishwa  kwa magendo.
Pia, Dk Mwakyembe alisema amewaagiza maofisa wa polisi kumtafuta raia wa Congo aliyepeleka mzigo huo bandarini, kwa lengo la kuusafirisha  kwenda  nchini Romania.

No comments:

Post a Comment