Friday, February 8, 2013

CAG APIGWA KUFULI

SERIKALI imewasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko katika Sheria ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma ya 2008, huku ikiongeza vifungu ambavyo vinapunguza nguvu ya Bunge katika kushughulikia taarifa ya Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Marekebisho hayo yamo kwenye Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria, namba 3 ya mwaka 2012 (The Written Laws - Miscellaneous Amendments Bill) uliowasilishwa bungeni jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.

Kwa mujibu wa Ibara ya 143 (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anawajibika kuwasilisha taarifa yake kwa Rais ambaye baada ya kuipokea atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha Bunge kilicho karibu.

Taarifa hiyo inabidi iwasilishwe katika kikao hicho kabla ya kupita siku saba tangu siku ile kilipoanza kikao hicho.

Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa baada ya ripoti hiyo kuwa silishwa bungeni itajadiliwa katika kamati tatu zinazosimamia Hesabu za Serikali kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi, kisha kuwasilisha taarifa zake bungeni katika muda zitakazopangiwa.

Kamati hizo za Bunge ni zile za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ambazo hufanya uchambuzi kisha kusoma taarifa zake ndani ya Bunge kwa hatua zaidi.

Hata hivyo, marekebisho yaliyowasilishwa Bungeni jana na Jaji Werema yanapendekeza kubadili utaratibu mzima wa kushughulikia taarifa hiyo, kwani yanaongeza vipengele, “vinavyoliwajibisha Bunge kwa Serikali” badala ya kinyume chake.

Serikali imeongeza vipengele vya ziada ambavyo vinazitaka kamati za Bunge zinapofanya uchambuzi wa ripoti ya CAG, kupeleka maazimio yake kwa Serikali ili “yatafutiwe majawabu” badala ya utaratibu wa sasa wa kupeleka hesabu zake bungeni.

Kimsingi Kamati za Bunge hufanya kazi kwa niaba ya Bunge, hivyo taarifa zake husomwa Bungeni na siyo kwingineko kama ambavyo marekebisho ya sheria yanataka kuelekeza.
Jaji Werema alisema: “Marekebisho haya yamefanywa ili kumwezesha Waziri wa Fedha kuwasilisha taarifa ya majibu ya Serikali ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali”.

Ikiwa Bunge litapitisha marekebisho hayo ni dhahiri kwamba Bunge halitakuwa tena na uwezo wa kuwawajibisha watendaji wa Serikali ambao watabainika kuhusika na upotevu wa fedha au kufuja fedha za umma, hivyo kupunguza uzito wa mjadala na uwezo wa wabunge kuhoji.

Kadhalika taarifa za LAAC, POAC na PAC kuhusu taarifa ya CAG na mapendekezo ya kamati hizo, yatajadiliwa sambamba na majibu ya Serikali. Hivyo hakutakuwa na nafasi ya Bunge kutekeleza wajibu wake wa kuisimamia Serikali kama inavyoainishwa katika Katiba.

Hatua hiyo ni sawa na kulifunga Bunge mikono kutokutekeleza wajibu wake kuhusu ripoti ya CAG, kwani kwa mujibu wa sheria halitaweza kujadili chochote hadi Serikali kupitia kwa Mlipaji Mkuu (Paymaster General) atakapokuwa ametoa majibu ya utetezi kuhusu kasoro katika ripoti hiyo.

source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment