Wednesday, January 23, 2013

Lowassa ataka Katiba Mpya ifafanue maana ya rushwa


WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa jana alitoa maoni kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba jijini Dar es Salaam, huku akitaka Katiba Mpya ieleze maana halisi ya rushwa ya uchaguzi ili kuondoa utata.
Mbali na hoja hiyo, Lowassa pia ametaka Katiba Mpya ifute adhabu ya kifo, iweke mgawanyo sawa wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji na itoe haki ya kupata elimu ya sekondari bure kwa kila Mtanzania.
Akitoa maoni kuhusu rushwa, Lowassa alisema,  “Katiba Mpya ifafanue rushwa ni nini katika uchaguzi.”
Alisema Katiba Mpya iwe na ibara inayofafanua ni kiasi gani cha fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia katika kampeni.
“Katiba Mpya iainishe ni matumizi gani ya lazima ambayo mgombea hawezi kukwepa kutumia fedha katika kampeni zake, mfano kuwakusanya watu kwenda kupiga kura nani azibebe gharama hizo,” alisema.

Lowassa alisema kwenye mfumo huo kila mtu atakuwa anapigania chama chake kupata kura nyingi ili wapate kura nyingi zaidi na kwamba hiyo itaondoa kikwazo kwa watu wenye fedha ambao hivi sasa wanawania uongozi.
Akizungumzia adhabu ya kifo, alisema Katiba Mpya ieleze kwamba hakutakuwa na adhabu ya kifo hapa nchini hata kwa kosa la kuua kwa kukusudia au uhaini.
“ Katiba ya sasa haisemi wazi kuhusu adhabu ya kifo, inazungumzia tu haki ya uhai, inazungumzia tu kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na uhai wake kulindwa,” alisema.
Kuhusu elimu, Lowassa alipendekeza Katiba Mpya itamke wazi kuwa elimu itatolewa bure kwa kila Mtanzania.Alisema kwenye majimbo mbalimbali wazazi wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za ada na kwamba wabunge ndiyo wamekuwa wakibeba mzigo huo kuwasaidia.
Kuhusu ardhi, Lowassa alitaka kuwe na kipengele katika Katiba Mpya kinachotoa nafasi sawa za kumiliki ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Lowassa ambaye anatoka katika eneo lenye wafugaji wengi alisema katiba ya sasa inawapa nguvu wakulima na kuwasahau wafugaji na kwamba wafugaji wamekuwa wakimbizi katika nchi yao.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment