Tuesday, January 22, 2013

Mkapa ajitosa sakata la gesi



RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameelezea kufedheheshwa kwake na mgogoro wa gesi, huku akiwataka wananchi na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Mtwara kusitisha harakati za maandamano na mihadhara.
Mkapa alitaka wakazi hao kuacha kulumbana na Serikali kuhusu suala hilo, badala yake wajiandae kukaa meza moja nayo kutafuta mwafaka kwa njia ya amani.
Katika tamko lake alilolitoa Dar es Salaam jana, Mkapa alisema: “Fujo, vitisho, kupimana nguvu na malumbano siyo masharti ya maendeleo.
“Nikiwa kama mwana - Mtwara na raia mwema, mpenda nchi, nimefedheheshwa sana na matukio haya ya siku za karibuni Mtwara. Kwa sababu hiyo natoa wito kwa wadau wote wa maendeleo ya Mtwara, kusitisha harakati hizi na maandamano na mihadhara.
“Badala yake wajipange kukaa pamoja katika meza moja,  kupitia historia, kutathmini mipango, kuchambua kwa kina mikakati ya utekelezaji wake, hatimaye kufikia mwafaka wa ujia wa maendeleo. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.”
Mkapa alisema mwenendo wa mazungumzo, maandamano na mikutano ya hadhara inayoendelea mkoani Mtwara, inaelekea kuashiria kuvunjika kwa amani hali aliyosema kuwa inajenga kutokuelewana kati ya viongozi wa vyama vya siasa na Serikali, wananchi na vyama vya siasa na wananchi na viongozi wa Serikali.
“Mtafaruku huu haufai kuachwa na kutishia usalama, mipango ya maendeleo siyo siri, mikakati na mbinu za utekelezaji wake siyo siri,” alisema Mkapa na kuongeza:
“Maelezo yake mazuri yanaweza kutolewa yakadhihirisha namna na kasi ambayo rasilimali zinawanufaisha wananchi wa eneo zilimo na taifa zima.”
Mkapa alisema hali hiyo ni tishio kwa wawekezaji wa ndani na nje, kwani mara zote hawapendi vurugu, fujo na vitisho.
Kauli hiyo ya Mkapa imekuja siku kadhaa tangu kuwapo kwa maandamano na vurugu zinazofanywa na baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanaopinga gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam.
Tayari viongozi kadhaa akiwamo Rais Jakaya Kikwete wametoa tamko juu ya suala hilo wakionya kuwa halikubaliki kwa kuwa rasilimali hiyo si kwa ajili ya wana Mtwara pekee.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliyalaani maandamano hayo akisema walioyaandaa wamelenga kuigawa nchi vipandevipande, Chadema kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kumbana waziri huyo ili aondoe udhaifu uliopo katika sekta ya nishati.
Desemba mwaka huu, maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka hapa kwenda Dar es Salaam.
Maandamano hayo yaliyoratibiwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party (TLP), APPT- Maendeleo, ADC, UDP na DP yakishirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo, zikiwamo Tandahimba na Newala  yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara Mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment