Friday, January 18, 2013

Kamati ya bunge yanusa ufisadi mikataba ya gesi


Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe 
KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma (Poac), imelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuwasilisha kwenye kamati hiyo mikataba iliyoingiwa na Serikali kuhusu ujenzi wa bomba la gesi la Mtwara hadi Dar es Salaam ili ipitiwe upya.

Mbali na uamuzi huo, kamati hiyo imeitaka Serikali itoe elimu kwa wakazi wa mikoa ya kusini kuhusu mradi huo ili kuondoa mgogoro uliokwishajitokeza.


Kamati hiyo ilitoa maagizo hayo jana baada ya wajumbe wake kubaini kuwa kuna makubaliano yasiyo rasmi baina ya Serikali na makandarasi wa bomba hilo, jambo ambalo linaweza kuitia hasara Serikali.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe alisema TPDC inapaswa kuwasilisha mikataba hiyo kabla ya kumalizika kwa kikao kijacho cha Bunge ili waweze kuipitia upya na kujiridhisha.
“Tumewaambia TPDC watuletee mkataba wa ujenzi wa bomba la gesi la Mtwara. Hii itasaidia kuangalia makubaliano yaliyoingiwa kati ya Serikali na mkandarasi, jambo ambalo linaweza kutusaidia kubaini kama una utata au la,” alisema Zitto.
Alisema hatua ya kupitia upya mikataba hiyo itasaidia kubaini upungufu uliopo na kuufanyia kazi, kabla ya kuanza mradi huo ili kuokoa fedha ambazo zingeweza kupotea kutokana na tatizo la ubovu wa mikataba.
“Lengo la kufikia uamuzi huo ni kuangalia mkataba huo kama umefuata hatua za kisheria au la, maana mkataba uko wizarani na TPDC hawana nakala, wakati ndiyo wanaosimamia mradi huo, sasa kuna usiri gani hapo?” alihoji Zitto.
Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu alisema kitendo cha TPDC kutokuwa na mkataba huo wakidai uko wizarani, kinaonyesha kuwa kuna jambo lisilo la kawaida.
Akizungumzia sakata la wananchi wa Mtwara kuandamana, Mangungu alisema kitendo kile kinatokana na Serikali kushindwa kuwaelimisha wananchi wa maeneo yanayopitiwa na mradi huo.

“Serikali ilipaswa kuwaelimisha wananchi wa Mtwara kuhusu gesi, hii ingesaidia kuamini kuwa mradi huo bado haujakamilika na wanapaswa kusubiri lakini wamekaa kimya, badala yake wananchi wanaamini kuwa umekamilika na kwamba hawawezi kunufaika na kitu chochote, jambo ambalo limesababisha waandamane,” alisema.

Mkurugenzi wa TPDC, Yona Kilagane alisema mkataba baina ya kampuni inayojenga bomba hilo na Serikali uko wizarani.

“Sisi hatuna mkataba wa ujenzi wa bomba hilo mkataba wake uko wizarani, kazi yetu ni kusimamia na kushirikiana na kampuni inayoendesha mradi kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo,” alisema Kilagane.
Mwaka jana, Serikali ilizindua ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 532 ambao utakamilika kabla ya mwaka 2014.
Kampuni zilizoiingia mkataba wa ujenzi wa bomba hilo ni Shirika la Maendeleo ya Teknolojia ya Petroli China, Shirika la Uhandisi wa Bomba la Petroli na Shirika la Uhandisi wa Bomba la Petroli la China.



Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment