Thursday, January 10, 2013

NYUMBA 19 ZACHOMWA MOTO KWA MAKUSUDI



NYUMBA 19  ambazo idadi ya wakazi wake haikujulikana mara moja zimeteketea kwa moto unaodaiwa kuwashwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa akishirikiana na polisi wa Kituo ch Staki Shari jijini Dar es Salaam.
Nyumba hizo zilijengwa katika Mtaa wa Vikongoro, Kata ya Chanika  Wilaya ya Ilala katika eneo ambalo linadaiwa kuwa na mgogoro.
Akisimulia tukio hilo, mkazi wa kitongoji hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Yusuph Kondo (80) alisema mchana wa jana alimwona Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa  akiwa na  kidumu cha mafuta na kwamba alielekea kwenye nyumba ya Zaituni Mguguli na mara baada ya kufika eneo hilo aliona moto ukiunguza nyumba.
Naye mtoto wa Zaituni aitwaye Ajuaye Twaha(10), alisema walifika mwenyekiti akiwa na askari na kumwamuru atoke nje  na kwamba alimuona askari akimwagia mafuta na kuwasha moto.
Akizungumza kwa masikitiko, Zaituni alisema samani za ndani, magodoro na Sh 900,000 alizopewa  na mtoto wake wa kwanza ili kumlipia ada mdogo wake ziliungua ndani ya nyumba hiyo.
Miongoni mwa wakazi waliopata hasara kutokana na  tukio la kuungua nyumba zao, ni Fikiri Hassan, Zuberi Kiiba, Asha Abdallah,  na Issa Salehe.
Ofisa Mtendaji wa mtaa huo, Ali Kambi, alipoulizwa juu ya tukio hilo alikiri  na kwamba lilitokana na mgogoro  wa ardhi.
Alisema waliochomewa nyumba wote walivamia eneo la mtu anayeitwa Nicolaus Malose aliyemilikishwa na kijiji tangu 2011.
Hata hivyo waathirika wa tukio hilo walisema eneo hilo ni lao tangu mwaka 1985.

Mkuu wa Kanda ya Kipolisi   Ilala, Marietha Minongi Komba alipoulizwa jana kuhusu  tukio hilo alisema hakuwa na  taarifa  za kuungua kwa nyumba na kwamba siku ya jana alizungumza  na Mkuu wa  Kituo cha Polisi Ukonga mara saba, lakini hakupata taarifa zozote.

Source:Mwananchi

No comments:

Post a Comment