SHAIRI KUTOKA KWA MDAU
MOLA MBARIKI MAMA!
Ya Rabbi Mola Rahima, mwenye kumiliki enzi,
Pokea yangu kalima, ewe usiye na mwezi,
Dua langu nalituma, kwa usiye ni vikwazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi.
Mola mbariki mama, kwa yake bora malezi,
Lolote nitalosema, halitoshi kumuenzi,
Alivyonilea vema, na kunifuta machozi
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Amenifunza hekima, vipi niishi na wenzi,
Na pia bora heshima, nisifate wapotozi,
Hii ni kubwa neema, gizani huwa kurunzi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Nilipopigwa na homa, udogoni hizo enzi,
Mama kucha husimama, kwa ule wangu ulizi,
Kwa zake nyingi huruma, humiminikwa machozi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Kumbatio lake mama, lilinipa utulizi
Kwa sauti yake njema, aliniimbia tenzi
Na kunifunza kusema, mie wake mwanafunzi
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Alinilaza kwa hima, niwapo na usingizi,
Japo awe anahema, kwa kuzidiwa makazi,
Hakika zake huduma, ni pendo lililo wazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Ni nini nimpe mama, kulilipa lake penzi,
Dhahabu kama mlima, ibebwe na wachukuzi,
Haitoshi ninasema, kwa huyu mwema mzazi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Beti hii nasimama, bila kufanya mapozi,
Machache niliyosema, mama kumpa pongezi,
Hakika yake karama, kuisahau siwezi,
Mola mbariki Mama, Mama ni wangu kipenzi
Shairi kukoka kwa mdau Mussa Msengi Gunda wa Gunda Foundation Tanzania
No comments:
Post a Comment