Ufaransa imekataa ombi la rais wa
Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize kusaidia kuwarudisha nyuma waasi
wanaotishia kuiangusha serikali yake, huku Marekani ikiamua kufunga ubalozi
wake nchini humo.
Wasiwasi umezidi kutanda nchini humo
wakati muungano wa waasi hao unaojulikana kama Seleka ukizidi kusonga mbele
kuelekea mji mkuu Bangui, kwa madai kuwa serikali imekiuka makubaliano ya amani
yaliyosainiwa mwaka 2007. Lakini rais Francois Hollande wa Ufaransa amekataa
ombi la rais Francois Bozize akisema kuwa muda wa kufanya hivyo ulikwisha.
Wakati
huohuo,Marekani kwa upande wake imetangaza
jana Alhamisi kuwa inasitisha shughuli zote katika ubalozi wake mjini Bangui,
na kwamba balozi wake na wafanyakazi wengine wa ubalozi huo walikuwa wameondoka
nchini humo. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Patrick
Ventrell, alisema uamuzi huo ulichukuliwa kwa kuhofia usalama wa wafanyakazi
hao, na kwamba hatua hiyo haihusiani kwa namna yoyote ile na uhusiano wa muda
mrefu wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo mawili. Marekani pia
iliwatahadharisha raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Hayo yanajiri wakati viongozi wa
kanda hiyo wakijaribu kuratibu makubaliano ya kusitisha mapigano na waasi
walikuwa wamesema wamesimamisha kwa muda, operesheni kuelekea mji mkuu, ili
kuruhusu mazungumzo kufanyika. Waasi hao wanataka serikali itekeleze
makubaliano ya kuwatawanya na kuwaingiza katika maisha ya kiraia.
"Wapiganaji wanataka pesa
walizoahidiwa ili kuweza kujiunga na jamii ya kiraia, programu ya kuwatawanya
ilihusu kuwanyang'anya silaha wapiganaji lakini yote hayo hayakutekelezwa na
ndiyo matatizo makubwa. Lingine ni kuundwa kwa ajira kwa waasi kwa lengo la
kuwaingiza katika maisha ya kiraia," alisema Thierry Vircoulon kutoka
shirika la kutatua migogoro la International Crisis Group, anafafanua madai ya
waasi hao.
No comments:
Post a Comment