Tuesday, December 11, 2012

UMOJA WA ULAYA WATUNUKIWA TUZO YA NOBEL



Umoja wa Ulaya umepokea tuzo ya amani ya Nobel leo mjini Oslo, ukitambuliwa na kamati ya tuzo hiyo, ambayo imetambua mchango wake wa kuendeleza utulivu na demokrasia.
 Kamati ya Nobel, yenye makao yake mjini Oslo, ilisema Umoja wa Nchi za Ulaya ulipewa tuzo hiyo kwa sababu ya jukumu lake la kuliunganisha bara Ulaya baada ya Vita vya Dunia vya Pili.
Umoja huo umewatuma marais wake watatu katika sherehe hiyo ya mjini Oslo kupokea tuzo hiyo ya mwaka 2012, ambayo wakosoaji akiwemo mshindi wa zamani Desmond Tutu wanasema haukustahili. Lakini mwenyekiti wa kamati ya Nobel, Thorbjorn Jagland amesema kamati yake haikukosea kuupa Umoja huo tuzo hiyo.
"Umoja wa Ulaya umekuwa nguzo muhimu katika michakato hii ya maridhiano. Umoja wa Ulaya umesaidia kuleta udugu kati ya mataifa na kuendeleza mikutano ya amani ambayo Alfred Nobel aliiandika katika wosia wake. Kwa hiyo tuzo hii ya amani inastahili na ni muhimu, na sote tunatoa pongezi zetu," alisema Thorbjorn.

No comments:

Post a Comment